Jesca Msambatavangu aweka nia tena Iringa Mjini

IRINGA: MBUNGE  wa Jimbo la Iringa Mjini anayemaliza muda wake, Jesca Msambatavangu, leo amechukua na kurejesha fomu ya kugombea tena nafasi ya ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hatua hiyo inaonesha dhamira yake ya kuendeleza kazi ya kulitumikia jimbo hilo kwa kipindi kingine.

Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu hiyo, Jesca amesema hatua hiyo inaakisi moyo wake wa kizalendo na mapenzi makubwa kwa wananchi wa Iringa Mjini ambao kwa miaka mitano wamekuwa sehemu ya mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali za maendeleo.

“Nimerudi tena kwa ajili ya kuendeleza kazi tuliyoianza. Naamini bado nina jukumu la kutimiza yale yote ambayo wananchi wetu wanayatarajia, kwa kushirikiana kwa karibu kama tulivyofanya awali,” amesema.

Katika kipindi chake cha uongozi, Jesca ametaja baadhi ya mafanikio ambayo Jimbo la Iringa Mjini limeyapata ikiwemo: Iringa kuimarika kama lango kuu la utalii wa kusini, kufunguliwa kwa Uwanja wa Ndege wa Irinha, na kuongezeka kwa fursa za kiuchumi.

Katika sekta ya afya ametaja ujenzi wa zahanati nne mpya, kuboreshwa kwa vituo vya afya, pamoja na Hospitali ya Frelimo.

Kwa upande wa sekta ya elimu ametaja ujenzi wa madarasa 130, shule mpya tano za msingi na nne za sekondari, pamoja na kuajiri walimu 410.

“Na chuo Kikuu cha Mkwawa kimepokea zaidi ya Sh bilioni 14 kwa maboresho,” amesema.
Kuhusu sekta ya maji na nishati amesema asilimia 97 ya wananchi sasa wanapata huduma ya maji safi, huku mitaa miwili tu ikiwa imebaki kuunganishwa na huduma ya umeme.

Alizungumzia pia haki za watoto na jinsia akisema mapambano ya ukatili wa kijinsia na watoto yanaendelea kwa kasi kubwa kwa kusimamia na kuchukua hatua madhubuti za kisheria dhidi ya wahalifu.

Jeska amesema endapo CCM itampa tena ridhaa ya kuipeperusha bendera ya chama hicho, ataongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati, hususani inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, huku akibeba maono mapya ya kulifanya Iringa Mjini kuwa kitovu cha ubunifu, biashara na huduma bora za kijamii.

“Moyo wangu bado uko Iringa Mjini, dhamira yangu haijabadilika. Nataka kushirikiana tena na wananchi kuijenga Iringa iwe kama Geneva, ikiwa na fursa zaidi zitakazowanufaisha wote,” amesema Jesca kwa msisitizo.

Kuhusu wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga alisema sehemu ya changamoto zao zimeshughulikiwa na zilizobaki zitamalizwa awamu inayokuja.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button