Watanzania washinda tuzo Kiswahili Safal ya Fasihi 2024

DAR ES SALAAM: TUZO ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika imetangaza washindi wa miswada ya mashindano ya mwaka 2024 katika hafla ya kufana iliyofanyika katika Chuo Kikuu Dar es Salaam Leo huku watanzania wakiibuka kidedea katika mashindano hayo ya tisa tangu kuanzishwa kwake 2015.
Tuzo hii, iliyoanzishwa na Dk Lizzy Attree na Dk Mukoma wa Ngugi mwaka 2014 ili kutambua uandishi kwa lugha za Kiafrika na kuhimiza tafsiri kutoka lugha hizo, baina ya lugha hizo na kwa lugha hizo, inafadhiliwa na kampuni ya Safal Group, kupitia ALAF-Tanzania na Mabati Rolling Mills-Kenya.
Mshindi wa kwanza katika kipengele cha Riwaya ni Mayasa Abdalla (Mtanzania) aliyejinyakulia kitita cha dola za kimarekani 5000 saa na zaidi ya sh milioni 12 kwa kuwasilisha mswada ujulikanao kama ‘Kitanzi cha Mauti.
Mshindi wa pili katika kipengele hicho ni Ali Masoud (Mtanzania) aliyewasilisha mswada ujulikanao kama ‘Nyaraka za Wafu’ huku akipata dola 2500 zaidi ya sh milioni 6 kama zawadi.
Katika kipengele cha Ushairi, mshindi ni Bashiru Abdalla (Mtanzania) mwenye mswada ujulikanao kama ‘Bure Ghali’ambaye alipata zawadi ya dola 5000 sawa na sh milioni 12 huku Mohamed Idrisa (Mtanzania) akishika nafasi ya pili kupitia mswada wake-‘Laana ya Uovu’ uliomzolea dola 2500.
Mshiriki kutoka Kenya, Edwin Omindu alitangazwa mshindi wa kipengele cha Hadithi Fupi kupitia mswada wake – ‘Mungu Hadanganywi’ huku akizawadiwa kitita cha dola 2500.
Waziri wa Utamaduni, Habari, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi alitoa pongezi kwa washindi wote kwa kazi nzuri na kuipa kongole Safal Group kwa kuwa mstari wa mbele katika kukienzi Kiswahili mwaka hadi mwaka.
“Mashindano haya yamekuwa maarufu na kuzidi kuvutia washiriki wengi wakiwemo baadhi kutoka katika mabara mengine kutokana na umuhimu wa lugha hii ya Kiswahili ambayo ni tunu yetu kwa hivyo lazima tujivunie na tukienzi ipasavyo,” amesema
Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za kukuza lugha ya Kiswahli kwani inatumika katika nchi nyingi za Kiafrika na baadhi ya nchi za ulaya wanakifundisha vyuoni ambayo ni fursa nzuri ya ajira kwa Watanzania.
Alipongeza pia Mkuki na Nyota Publishers na Africa Poetry Book Fund ambao ni wachapishaji wa miswada iliyoshinda, huku akitoa wito kwa mashirika mengine yajitokeze kuunga mkono jitihada hizi za kukienzi Kiswahili.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Tanzania, Ashish Mistry alisema kampuni ya Safal Group ambayo ni kampuni mama ya ALAF Tanznaia na Mabati Rolling Mills ya Kenya, imeendelea kudhamini tuzo hizo kutokana na ukuajia wake mwaka hadi mwaka na umuhimu wa Kiswahili katika kuunganisha bara la Afrika.
Mwenyekiti wa majaji wa mashindano ya mwaka 2024, Dk Salma Hamad, wa Chuo Kikuu Huria, Tanzania, alisema “Miswada ilikuwa mingi hata hivyo tumeburudika vya kutosha kwa sababu tumesoma kazi zilizoandikwa na kusukwa kiubunifu na tumejifunza kwamba kuna hazina kubwa ya vipaji vya uandishi wa fasihi ya kiswahili. Vikiendelezwa fasihi ya Kiswahili haitafilisika.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Tuzo hii, Bw. Abdilatif Abdalla, aliongeza, “Ni jambo la kufurahisha mno kuona kwamba tangu mashindano yalipoanzishwa mwaka 2015, bado Tuzo hii inaendelea kuwavutia washiriki kutoka nchi mbalimbali na kwa idadi kubwa. Pia kiwango cha ubora wa miswada inayoshindanishwa kinaongezeka kila mwaka, na kwa hivyo kuitajirisha Fasihi ya Kiswahili.”



