Halmashauri ya Mji Handeni yatoa mikopo mil 588/-

Halmashauri ya Mji Handeni imetoa Sh Milioni 588 kwa vikundi 109 vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu kwa kipindi cha miaka minne.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Wakili Marium Ukwaji amesema kuwa fedha hizo zimetolewa kwa mfululizo kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2024/2025.
Amesema mikopo hiyo imetolewa kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa mujibu wa Waraka wa Serikali, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la kuwainua kiuchumi wananchi kutoka makundi maalum.
“Wanufaika wa mikopo hiyo ni Vijana (46), Wanawake (109), na Watu Wenye Ulemavu (32) ambao wamejiunga kwenye vikundi na hivyo kutumia mikopo hiyo kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kiuchumi na kujiongezea kipato,” amesema Ukwaji.
Vile vile amesema mikopo hiyo imelenga kusaidia miradi ya uzalishaji mali ikiwemo kilimo, ufugaji, usindikaji wa mazao, biashara ndogondogo na shughuli nyingine za kiuchumi zenye lengo la kuongeza kipato cha wanufaika na familia.
Aidha Mkurugenzi huyo amesema Halmashauri itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa vikundi kupata mikopo kwa wakati, sambamba na kutoa elimu ya ujasiriamali ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa tija.
“Tunapenda kuona vikundi hivi vikikua na kuwa sehemu ya mabadiliko ya kiuchumi Handeni. Tunasisitiza marejesho kwa wakati ili vikundi vingine viweze kunufaika pia,” alisema.
Kwa upande wao, baadhi ya wanufaika wameeleza kuwa mikopo hiyo imekuwa mkombozi katika maisha yao, ikiwasaidia kuanzisha biashara ndogo, kulipa ada za watoto na kuboresha makazi yao.
Halmashauri ya Mji Handeni inasisitiza ushiriki wa vikundi zaidi kutoka kata zote, huku ikiendelea kutoa elimu kwa maafisa maendeleo ya jamii na viongozi wa mitaa kuhusu umuhimu wa mfuko huu wa maendeleo kwa makundi maalum.