Rais Samia asema Kiswahili daraja la maendeleo

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Lugha ya Kiswahili ni daraja la maendeleo.
Alisema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Umoja wa Visiwa vya Comoro yaliyofanyika katika Uwanja wa Malouzini Omnisport mjini Moroni jana.
Rais Samia alisema eneo la kusini mwa Afrika limegawanywa kuendana na lugha za watawala wa kikoloni na kuna mataifa yanazungumza Kiingereza, Kifaransa na wengine Kireno lakini Kiswahili ni lugha ya Kiafrika inayoweza kuunganisha mataifa hayo.
Alisema Kiswahili ni daraja la maendeleo kwa kuwa ni lugha ya mawasiliano, elimu na biashara kati ya mataifa hayo.
Rais Samia ameomba Kiswahili kifundishwe shuleni na kitambulike nchini Comoro ili kujenga na kuimarisha umoja uliopo kati ya Tanzania na nchi hiyo.
Alisema Tanzania ipo tayari kusaidia kutoa walimu na vifaa vya kufundishia ili kufanikisha hilo na akasema Kiswahili ni urithi wa pamoja wa mataifa hayo.
“Tukumbuke kwamba Kiswahili ni urithi wetu wa pamoja na ni daraja la maendeleo baina yetu,” alisema Rais Samia.
Siku ya Kiswahili Duniani
Novemba 23, 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilitangaza Julai 7, ya kila mwaka kuwa ni Siku ya Kiswahili Duniani.
Unesco ilipitisha uamuzi huo wakati wa mkutano wa nchi wanachama wa shirika katika makao makuu yake, Paris, Ufaransa. Utekelezaji ulianza mwaka 2022 hivyo mwaka huu ni maadhimisho ya nne.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi alisema Kiswahili ni tunu ya taifa.
Profesa Kabudi alisema lugha hiyo ni miongoni mwa lugha saba zilizotengewa siku ya kuadhimishwa na ina wazungumzaji takribani milioni 500 duniani.
Alisema serikali kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) imeandaa kanzidata ya wataalamu wa Kiswahili ili kubaini uwezo wa nchi kushiriki katika kueneza matumizi na maendeleo ya Kiswahili ndani na nje ya nchi kupitia huduma za ukalimani, tafsiri, ufundishaji kwa wageni pamoja na uandishi wa vitabu.
Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kwa wageni ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa kukipeleka kimataifa.

Alisema Bakita katika utoaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo diaspora wa kufundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni, tayari imewafikia diaspora 495.
Profesa Kabudi alisema diaspora hao wamefundisha wageni 266 wakiwemo 68 Italia, Ufaransa 148, Austria 23 na Nigeria 27.
Alisema pia Bakita imesajili vituo 51 vya kufundisha Kiswahili kwa wageni, 19 viko nje ya nchi na vituo 32 viko ndani ya nchi.
Bakita
Katibu Mtendaji wa Bakita, Consolata Mushi alitoa rai kwa wananchi hasa vijana wazungumze lugha ya Kiswahili fasaha kila wakati ili lugha hiyo iweze kuenea na kuzalisha misamiati mingine mipya.
Consolata alisema hayo wiki iliyopita alipozungumza kwenye kipindi cha mizani kilichorushwa na kituo cha televisheni cha Taifa cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1).
“Ile dhana ya kwamba msamiati wa Kiswahili ni mchache na hautoshelezi ni dhana potofu, Kiswahili kina msamiati wa kutosha kwa pande zote katika maeneo yote na hakuna upungufu,” alisema.
Consolatha alitoa mwito kwa wazee wanaofahamu Kiswahili kwa ufasaha wawasimamie vijana wasiharibu maneno ya Kiswahili kwa sababu ya kukua kwa teknolojia.
Tataki
Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), Profesa Aldin Mutembei alisema ni muhimu kwa wanafunzi wajifunze Kiswahili fasaha na wakitumie ili waweze kufundisha lugha fasaha katika mataifa yasiyotumia lugha hii.
Pia, aliwahimiza wanafunzi wajenge utamaduni wa kujifunza lugha za mataifa mengine yaliyoendelea kama vile Kireno, Kifaransa, Kichina ili kuchangamkia fursa za ukalimani na utafsiri zilizopo nje ya nchi hivyo kuongeza ajira.
“Kuna ajira nyingi katika nchi za SADC (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika) hapa kwetu hatuna wazungumzaji wengi wa Kireno lakini hizo ndio fursa za kujiajiri na kuwa wakalimani ni muhimu kuweka mkazo katika lugha nyingine,” alisema.
Profesa Mutembei ambaye pia ni mhadhiri wa fasihi katika taasisi hiyo, alisema serikali imejitahidi kuwekeza katika balozi na wawakilishi wa Tanzania kwa kuweka wataalamu wa kufundisha Kiswahili na mwaka huu serikali imeongeza bajeti ya Bakita ili kuwawezesha wataalamu kufundisha lugha nje ya nchi.
Alisema maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yamesaidia mataifa mengine kukifahamu zaidi na kupitia makongamano, maadhimisho yanayofuatiliwa duniani imesaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojifunza Kiswahili katika vyuo vikuu nchini.
“Kiswahili kimeleta tija, watu wanakuja kutalii hata kama hawajifunzi lugha lakini wanajifunza maneno na utamaduni kwa hiyo ni moja ya faida nchi inajenga uchumi,” alisema.
Mdhahiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Dk Mussa Hans alisema ni muhimu waandishi wa habari watumie kamusi itakayowasaidia kufahamu maana ya maneno.
“Unaweza kutumia Kiswahili kuelezea taaluma ya sheria, masuala ya kilimo, masuala ya uchumi kwa hiyo sisi tunaitumia fursa ya Kiswahili katika masuala ya taaluma, wanafunzi wetu wanapata mada nyingi kwa ajili ya kufanya utafiti wao katika maendeo mbalimbali yanayohusu lugha na utamaduni wa Mswahili,” alisema Dk Hans.
Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Alphonsina Ambrose alisema chuo hicho kinaanzisha programu ya Shahada ya Umahiri wa Kiswahili.
“Kwa mara ya kwanza chuo kikuu cha Mzumbe kitakuwa na shahada ya Kiswahili ya umahiri na si tu shahada ni shahada ambayo utaweza kusoma pia ukiwa huko ulipo, si lazima ufike, itakuwa katika mtandao au kwa anayetaka utakuja moja kwa moja, tunataka kila mmoja Kiswahili kimfikie kwa gharama nafuu,” alisema Ambrose.
Imeandikwa na Eva Sindika, Ramla Hamidu na Shakila Mtambo.



