Asilimia 85 waajiriwa sekta ya mafuta, gesi ni wazawa

DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Kudhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema ushiriki wa nafasi ya Watanzania unaongezeka na sasa asilimia 85 ya ajira katika sekta hiyo zinashikilia na wazawa.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Charles Sangweni akiwa katika banda la mamlaka hiyo kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba.
Alisema kiwango hicho kumeongezeka kutoka asilimia 55 iliyokuwa awali na kuwa hiyo imetokana na uzoefu,uelewa na Watanzania kuchangamkia fursa za masomo ya fani hiyo ambayo yananafadi kubwa ya ajira.
Watanzania wameongeza uzoefu kwenye sekta hii lakini pia uelewa vimeo ngezeka. Awali meli za utafiti na utafutaji mafuta na gesi zilikuja na wafanyakazi kutoka nje ya nchi lakini sasa ,wazawa wako ndani ya timu hizo za wataalamu ni hatua kubwa hii na ni jambo la kujivunia,”alisema Sangweni.
Alisema akizungumzia mipango ya PURA kwa sasa na siku zijazo,Sangweni alisema wako kwenye maandalizi ya kuchimba visima vitatu katika eneo la Mtwara, huku ushiriki wa Watanzania katika vitalu hivyo ukifika asilimia 40.
Alisema kati ya kampuni 10 zinazofanya utafiti wa mafuta na gesi nchini, sita zinamilikiwa na Watanzania na hiyo imetokana na juhudi zinazofanywa na serikali kuboresha mazingira ya fursa mbalimbali .
Alisema katika nafasi za uongozi ndani ya sekta, karibu asilimia 95 zinashikiliwa na Watanzania.
“Hatua hii ni mfano na dhamira ya dhati ya serikali kuhakikisha rasilimali zetu zinawanufaisha wananchi,” alisema Sangweni.
Katika hatua nyingine Sangweni ameipongeza serikali kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na ushirikishwaji wa Watanzania katika miradi ya kimkakati, akisisitiza kuwa PURA itaendelea kuhakikisha kila hatua ya maendeleo inawagusa wazawa moja kwa moja.
Akizungumzia agenda ya nishati safi ya kupikia,Sangweni alisema PURA inajivunia utekelezaji wa agenda ya hiyo iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwani imeanza kutekelezwa kwa vitendo na kuleta tija.
“Mwitikio wa wananchi kuhusu nishati safi ni mkubwa na tumejipanga kuhakikisha utekelezaji wake haumwangushi Rais Samia.
Alisema kupitia maonesho hayo ya sabasaba mwamko wa wananchi wa uelewa wa kutumia nishati hiyo ni mkubwa na unazidi kuongezeka na hiyo ni ishara kuwa somo limeeleweka kwa wahusika.
Alisema PURA imekuwa mshiriki wa kudumu wa maonesho hayo tangu mwaka 2017 na kwamba kila mwaka kumekuwa na maboresho ya kimkakati katika ushiriki wao.
Kwa mwaka huu, maboresho ya maonesho hsyo ni pamoja na matumizi ya mifumo ya kidigiti na ongezeko la wananchi na washiriki wanaotembelea banda la PURA.
Sangweni alisema wananchi na wadau wanaotembelea banda hilo wanauliza maswali ya msingi kuhusu uelewa wa sekta ya mafuta na gesi lakini pia kupokea maoni, changamoto yanayosaidia kuboresha utendaji wa PURA.



