Tabianchi Yatikisa Kilimo cha Mwani

KILIMO cha Mwani kimekuwa kama pumzi mpya ya uchumi katika ukanda wa pwani, hasa Zanzibar na mikoa ya Lindi, Tanga na Pwani. Tofauti na mazao mengine ambayo hustawi ardhini, mwani hustawi chini ya maji ya bahari. Hii si tu inaupa utambulisho wa kipekee, bali pia inaifanya shughuli hii kuwa na changamoto na fursa zinazotofautiana kabisa na kilimo cha kawaida.
Wakulima wa mwani, wengi wao wakiwa wanawake wa vijijini, wameanza kuiona bahari kwa jicho jipya. Si tena mahali pa uvuvi pekee au mapumziko, bali chanzo cha kipato halali na kilichojaa matumaini. Mwani unaleta chakula mezani, unalipia ada za watoto, na umebadilisha kabisa namna watu wanavyotazama maisha ya baharini.
Abdullah Mahzumi kutoka Kampuni ya Mwani Zanzibar (ZASCO) anasema wazi kuwa kilimo hiki si shughuli ya kawaida ya uzalishaji tu ni njia ya maisha.Kuna aina mbili kuu za mwani wanaokabiliana nao kila siku: ule wa chakula na mbolea unaookotwa na maji kuusukuma pwani, na ule unaopandwa kwa mikono ya wakulima ndani ya bahari, aina kama cottonii na spinosum. Hii kazi ya kupanda mwani huhitaji mbinu sahihi, na si kila mtu anaweza kuifanya bila mafunzo.
Mara nyingi, wakulima hujiandaa kwa msimu wa kupanda kupitia semina na mafunzo wanayopata kutoka kwa taasisi mbalimbali. Hapo hujifunza namna ya kuchagua mbegu bora, kupanda kwa usahihi, kuvuna kwa wakati, na muhimu zaidi kuhifadhi mwani kwa njia salama ili kulinda ubora wake. Wakati mwingine, wakulima huingia baharini asubuhi na mapema, wakati mawimbi yakiwa ya wastani, wakichuchumaa juu ya kamba zilizofungwa kwenye vijiti vilivyopigiliwa kwenye sakafu ya bahari, wakipandikiza vipande vya mwani kwa mikono yao.
Lakini hata kazi hii yenye neema haijakosa misukosuko. Mabadiliko ya tabianchi yameanza kubadili upepo wa matumaini kuwa mashaka. Mvua zisizotabirika huanza kunyesha ghafla, wakati mwani ukiwa tayari kwa kuvunwa. Maji ya mvua yanapoingia kwenye mwani kabla ya kukaushwa, huuweka katika hatari ya kuoza au kushambuliwa na fangasi. Hali hii inawakatisha tamaa wakulima wengi ambao walikuwa wameweka matumaini yao yote kwenye msimu mmoja.
Kuna pia tatizo la kemikali zinazotumika majumbani, hasa dawa za kuua mbu, kuingia kwa bahati mbaya kwenye maeneo ya kuhifadhia mwani. Matokeo yake, mwani unapoteza ubora wake na kushindwa kuuzwa. Wapo ambao bado huhifadhi mwani kwenye maeneo yenye unyevunyevu, au hufunika kwa vifaa visivyofaa kama karatasi za barua au vyandarua vya zamani, bila kujua kuwa wanaharibu jasho lao wenyewe.

Licha ya changamoto hizi, mwani umeendelea kusimama kama zao la matumaini. Wajasiriamali wadogo wameanza kugeuza mwani kuwa sabuni, mafuta ya ngozi, unga wa lishe, na bidhaa za mapishi. Mchakato huu wa kuongeza thamani umekuwa njia mpya ya kujitegemea, na umefungua milango ya ubunifu kwa wanawake na vijana wengi wa pwani.
Serikali nayo haikukaa kimya. Imechukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa wakulima wanapata bei nzuri ya mwani. Zamani walikuwa wakinyonywa na wanunuzi binafsi waliokuwa wakiwanunulia kwa bei ya chini mno. Sasa, serikali imenunua mwani kwa bei ya juu zaidi, hali iliyoongeza motisha kwa wakulima na kuifanya kazi hii kuonekana tena kama ya heshima.
Katika juhudi za kuondokana na kuuza mwani ghafi, serikali imejenga kiwanda cha kuchakata mwani Pemba. Hatua hii inaleta matumaini mapya ya kuingiza fedha za kigeni kupitia bidhaa zilizosindikwa si tena malighafi isiyo na thamani kamili.
Mwani hauwezi tena kuchukuliwa kama zao la kawaida. Kwa maelfu ya familia zinazoutegemea, ni zaidi ya kilimo ni njia ya kujenga maisha. Ndani ya maji haya ya chumvi, chini ya jua la ukanda wa pwani, wakulima wa mwani wanapambana na mazingira, wanatengeneza fursa, na kwa kila kipande kidogo cha mwani wanachopandikiza, wanapandikiza pia matumaini yao ya kesho bora.
SOMA: Mikakati inahitajika kupata soko la mwani EA



