Mikakati inahitajika kupata soko la mwani EA

TANZANIA ni nchi pekee kati ya nane wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inayozalisha zao la mwani kwa wingi kuliko taifa lolote ndani ya kanda.
Zao hilo ambalo linazalishwa kwa wingi kwenye Bahari ya Hindi Zanzibar hivi karibuni limepata soko kubwa ndani na nje ya nchi hususani Ulaya baada ya kujua umuhimu wa zao hilo kama lishe katika mwili wa binadamu.
Ni vizuri wataalamu wa lishe wa Tanzania wakatoa elimu ya umuhimu wa mwani kama lishe ya mwanadamu ili kuziamsha usingizini baadhi ya nchi zinazolichukulia ‘poa’ zao hilo.
Tunashauri katika utoaji wa elimu hiyo, wawepo wataalamu wa lishe wa nchi zote nane za EAC ili somo la lishe kuhusu mwani liende kwa haraka katika nchi zote kwa wakati mmoja.
Wakati akitoa hotuba ya kulivunja Baraza la Wawakilishi ambapo kisheria litavunjwa rasmi Agosti 13, Rais Dk Hussein Mwinyi alisema kutokana na kujua umuhimu wa zao hilo, serikali yake imeweka jitihada za kuimarisha ukulima wa zao hilo.
Alisema jitihada hizo zinalenga kukuza na kuimarisha uzalishaji wa zao hilo kwa kuwapa vifaa, taaluma na kuwajengea mazingira bora wakulima wa mwani ili kuhakikisha wanafaidi kazi za mikono yao.
Ni vyema Tanzania na Kenya kama wanachama wa EAC kuwa na kiwanda angalau kimoja cha kusanifu mwani kwa kuwa ni wanachama pekee wenye bahari.
Rais Mwinyi alisema Zanzibar imepata mafanikio kwa kuimarisha kilimo cha mwani ambapo uzalishaji wa zao hilo umeongezeka kwa asilimia 124.6 kutoka tani 8,785 za Sh bilioni 5.39 mwaka 2020 na kufikia tani 19,716 za Sh bilioni 16.14 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 124.6.
Tunazihimiza nchi zote wanachama wa EAC kuwa uwekezaji mkubwa katika zao hili una mafanikio mengi yakiwemo upatikanaji wa fedha za kigeni kwani tayari mahitaji yake huko nje ya Afrika ni makubwa.
Ni ukweli kuwa kilimo cha mwani kinaweza kulimwa katika nchi tatu za EAC ambazo ni Tanzania, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa kuwa mataifa hayo yanaguswa na Habari.
Tunatarajia mataifa hayo kushirikiana kufanikisha kilimo cha mwani katika EAC ili kupanua uzalishaji wa zao hilo na kulipatia soko kubwa ndani ya jumuiya na Afrika kwa ujumla.
Mategemeo yetu ni kwamba kwanza nchi za EAC zishirikiane katika kufanikisha soko kubwa la mwani unaozalishwa Tanzania na baada ya kupata mafanikio katika hilo, zishirikiane kuzalisha ili kuwa na mwani kutoka Afrika Mashariki.