Chalamila: dini, siasa haviwezi kutengana

DAR: Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema kuwa siasa na dini ni taasisi zinazogusa maisha ya kila mtu kwa namna ya karibu na haziwezi kutenganishwa katika muktadha wa jamii yoyote inayotaka maendeleo na mshikamano.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mkutano wa viongozi wa dini, Chalamila alisema hakuna binadamu anayeweza kuishi maisha ya upande mmoja pekee – iwe ni ya kisiasa au kiroho – kwani mifumo hiyo huingiliana na kuathiriana kwa kiasi kikubwa.

Alisisitiza kuwa kabla mtu hajafanya uamuzi mkubwa maishani, ni lazima afikirie athari zake kwa dini yake, jamii na taifa, kwa sababu kila hatua huleta matokeo yanayoathiri watu wengi.

Chalamila alitolea mfano mataifa kama Iran na Israel ambako dini imekuwa sehemu ya mfumo wa kisiasa, jambo linalodhihirisha kuwa dini si taasisi ya pembeni bali ni kiungo muhimu cha maamuzi ya kitaifa.

Alieleza kuwa kuna nyakati dini na siasa hutofautiana (muachano), lakini pia kuna maeneo mengi ambapo zinakutana na kushirikiana (mukutano) – hasa katika ujenzi wa maadili, uongozi na maendeleo ya jamii.

Aidha, alisisitiza kuwa binadamu hujengwa na mifumo mbalimbali kama familia, dini, siasa na elimu, hivyo ni muhimu kuhakikisha mifumo hiyo inafanya kazi kwa pamoja katika kujenga kizazi chenye maadili.

Akizungumzia nafasi ya lugha katika mshikamano wa kitaifa, Chalamila alisema Kiswahili ni chombo muhimu kinachotoa mamlaka ya sauti kwa jamii, na ni utambulisho wa kitaifa unaowafanya Watanzania kuwa wamoja.

“Kiswahili si lugha tu, ni mamlaka. Mtu asiye na lugha hana sauti. Lugha inatufanya kuelewana, kujenga hoja na kujenga Taifa,” alisema Chalamila huku akitoa wito wa kuitunza lugha hiyo.

Kwa upande wao, viongozi wa dini walitumia mkutano huo kutoa wito wa kudumisha amani na mshikamano hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, wakisisitiza kuwa siasa isitumike kama chanzo cha chuki au migawanyiko.

Mchungaji Boniface Mwamposa alisema viongozi wa dini wanapaswa kuhubiri amani kama Kristo alivyofanya, kwa kuwa amani huanzia kwenye roho za watu na madhabahu zinapaswa kuwa sehemu ya kuijenga.

Shehe Mkuu wa Mkoa, Walid Alihad, alieleza kuwa mjumuiko wa viongozi wa dini kujadili masuala ya amani ni neema kwa Taifa, na akasisitiza umuhimu wa hekima, heshima na uvumilivu katika nyakati za mvutano wa kisiasa.

Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, aliahidi ushirikiano wa vyombo vya dola na viongozi wa dini katika kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani, akiwataka Watanzania kuweka mbele maslahi ya Taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button