Mtoto wa mwanariadha ajitosa urais SRT

ARUSHA: KATIBU Mkuu wa Chama Cha Riadha Mkoa wa Arusha (RT) Rogath Stephen ni miongoni mwa wagombea wa nafasi ya urais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (SRT).

Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika agosti 16 mwaka huu jijini Mwanza.

Stephen ni mtoto wa tatu wa gwiji wa riadha nchini, John Akhwari aliyetamba katika mchezo wa riadha katika miaka ya 1962 na mwaka 1968 alionekana shujaa kwenye michezo ya Mexico Olympic na kuiletea sifa nchi ikiwemo ushindi na kufanikiwa kupata medali.

Katibu huyo ambaye ni Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi Kituo Kikuu cha Polisi Arusha ameamua kujitosa katika Kinyang’anyiro hicho akiwa na wagombea wengine watatu akiwemo mtetezi wa kiti hicho, Silas Isangi.

Wengine walioamua kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi mbali ya Stephen na Isangi wengine ni pamoja na aliyekuwa mwanariadha mkongwe wa mbio ndefu nchini, Juma Ikangaa na Williamu Karage ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho hilo.

Kwa mujibu wa Katiba mpya wa SRT iliyopitishwa mapema mwaka huu na Baraza la Michezo Nchini (BMT) Ibara ya 29 inasema kuwa ili uwe kiongozi wa shirikisho hilo lazima uwe umewahi kuwa mwanariadha wa kitaifa ama kimataifa,uwe kocha wa riadha, uwe umewahi kushiriki kozi mbalimbali za riadha na uwe na udhoefu wa uongozi ngazi ya mkoa kwa muda usiopungua angalau miaka mitano.

Mmoja wa wanariadha wakongwe nchini, Marcelina Gwandu amesema kuwa Katiba mpya ya SRT imetungwa kwa lengo la kuendeleza mchezo huo nchini ikiwa ni pamoja na kutaka Shirikisho hilo kuongozwa na wanariadha wenye kuujua mchezo huo ipasavyo na wagombea wasiokuwa na sifa hizo wasiweze kupata nafasi.

Gwandu ambaye alishiriki michezo ya Olympic 1980 nchini Moscow Urussi alisema timu ya wataalamu waliteuliwa kuirekebisha katiba hiyo na kwenda na wakati hakika wameitendea haki katiba hiyo kwani wameweka vitu vya msingi vyenye kuendeleza mchezo huo kwa maslahi ya wanariadha na nchi kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button