Tetemeko la 7.3 lapiga Alaska

ALASKA : TETEMEKO kubwa la ardhi lenye ukubwa wa 7.3 katika kipimo cha Richter limetokea katika pwani ya jimbo la Alaska, nchini Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Utafiti wa Jiolojia la Marekani (USGS), tetemeko hilo lilitokea majira ya saa sita mchana kwa saa za eneo hilo, likiwa na kitovu chake takriban kilomita 87 kusini mwa mji wa kisiwa cha Sand Point.
Mara baada ya tukio hilo, mamlaka zilitoa tahadhari ya uwezekano wa kutokea kwa tsunami katika maeneo ya kusini na rasi ya Alaska, ingawa baadaye tahadhari hiyo iliondolewa.
Wakazi wa maeneo ya karibu na bahari walipewa maelekezo ya kuchukua tahadhari kwa kuondoka kwenye maeneo hatarishi ili kujikinga na madhara ya tetemeko hilo. SOMA: Waliokufa kwa tetemeko la ardhi wafikia 161 Japan
Hii si mara ya kwanza kwa eneo hilo kukumbwa na matetemeko makubwa, kwani mwezi Julai mwaka 2023, tetemeko la ukubwa wa 7.2 liliikumba rasi ya Alaska, ingawa halikusababisha uharibifu mkubwa.



