BBT yashika kasi
WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe amezindua Kampeni ya Mali Shambani kuhamasisha vijana kuingia kwenye kilimo biashara.
Bashe pia, amezindua mfumo wa huduma za ugani kidijiti (Ugani Kiganjani) itakayowezesha wakulima kupata huduma za ugani kirahisi kutoka kwa maofisa ugani waliosajiliwa.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni na mfumo huo katika Kituo cha umahiri cha Mtanana kilichopo Kongwa mkoani Dodoma alisema katika kutekeleza kampeni hiyo watakwenda vijijini ili kuzungumza moja kwa moja na wakulima.
“Tunataka kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na wakulima sisi wizara ya kilimo, kwa hiyo tunatumia njia mbalimbali rasmi kwa sababu tunafanya kazi na halmashauri za kila kijiji na tutaenda kule vijijini mwaka mzima,” alisema Bashe.
Kuhusu mfumo wa Ugani Kiganjani alisema wakulima wote watakuwa nao kwenye simu na kwamba ulianza kutumika miaka mitatu iliyopita na sasa umefikia wakulima milioni na lengo ni kusajili wakulima milioni saba.
“Sasa tunawasajili katika mfumo maofisa ugani wa serikali na vijana waliosoma shughuli za ugani ambao hawajaajiriwa, tutawaingiza kwenye mfumo ambao mkulima atakuwa nao kwenye simu yake na hii itakuwa huduma ya bure kwa mkulima kumtambua ofisa ugani, huyo ofisa ugani atakuwa ni yule aliyethibitishwa, tunataka kuwaondoa makanjanja kwenye sekta ya kilimo,” alisema Bashe.
Kituo cha umahiri Bashe alisema kituo cha umahiri cha Mtanana kitaboresha teknolojia za vijana 15 na zikifikia kiwango cha kwenda sokoni serikali itaziunga mkono kuzipeleka sokoni.
“Najua shida ya nchi yetu mnaweza kuwa na teknolojia hapa badala ya kuchukua mkasema tangaza tenda kwenye hii hakutakuwa na tenda teknolojia yote itakayopatikana kama tunaihitaji tunainunua moja kwa moja kutoka kwao kama serikali badala ya kusumbuka kwenda kwingine,” alisema.
Bashe alisema kutakuwa na vituo vingine vitano kama hicho nchini na kimojawapo kitakuwa Kigoma ambacho kitahusiana na mazao yakiwemo ya mihogo na tangawizi.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua kituo hicho Agosti 8, mwaka huu na baada ya tukio hilo Makao Makuu ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) yatahamia Mtanana.
“Ofisi ya Mkurugenzi wa NFRA ipo hapa wote mnahama, kule Dodoma mjini mtasema hakuna nyumba, hapa kuna nyumba za kukodi vijijini, hapa walimu wa shule ya msingi wanakodi nyumba hapa na nyie mtakodi nyumba
mhamie hapa,” alisema Bashe.



