Waratibu Tasaf kusimamia fedha za miradi

TANGA: Waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mkoani Tanga wametakiwa kusimamia miradi ya miundombinu inayotekelezwa na mradi huo inakamilika katika viwango vyenye ubora.
Kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya kimiundombinu kwenye maeneo ya walengwa ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kupeleka maendeleo.

Akiongea wakati wa kikao kazi cha waratibu wa mpango huo mkoa waTanga Kaimu Katibu Tawala mkoani hapa, Amina Said hapo jana alisema kuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia kuonyesha namna sahihi ya matumizi ya fedha hizo.
Hivyo aliwataka kusimamia kwa ukamilifu miradi hiyo ili iweze kujibu Changamoto zilizipo kwenye jamii kupitia miradi hiyo.
“Kuna miradi kama ya ujenzi wa miundombinu ya afya ,elimu maji na barabara hii yote inagusa jamii hivyo ni muhimu kuhakikisha inakamilika katika viwango bora lakini kwa wakati,” alisema Kaimu RAS.

Hata hivyo Meneja wa TASAF makao makuu, Salome Mwakigomba alisema kuwa Mkoa wa Tanga unapokea Sh milioni 800 kwa ajili ya wanufaika wa mpango huo kila baada ya miezi mitatu.
Alisema kuwa kupitia mpango huo wamewezesha maisha ya walengwa kuweza kuimarika ikiwemo kutoa fursa za elimu,pamoja na kiuchumi .
Naye Mratibu wa TASAF Tanga, Ramadhani Ally alisema kuwa jumla ya wanufaika 38952 sawa na asilimia 56%ya walengwa wameweza kuanzishiwa biashara ndogondogo na kujiongezea kipato.




