Ruzuku ya chanjo, utambuzi kuwezesha biashara ya mifugo kimataifa

DAR ES SALAAM: UWEKEZAJI wa serikali kwenye sekta ya mifugo kwa kutoa ruzuku ya chanjo na utambuzi wa mifugo utasaidia kupatikana kwa ithibati ya kufanya biashara ya mifugo na mazao yake kwenye masoko ya ndani na ya kimataifa kutoka Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH).
Hayo yamebainishwa jana na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Edwin Mhede wakati akikagua utekelezaji wa Kampeni ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo katika Kijiji cha Soera wilayani Kondoa, Mkoa wa Dodoma.
“Leo tumekabidhi pikipiki 31 kwa maofisa ugani ili waweze kutekeleza kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo, serikali imetoa ruzuku ya chanjo ya asilimia 50 kwa ng’ombe, mbuzi na kondoo na asilimi 100 (bure) kwa chanjo ya kuku kwahiyo chanjo hii itaongeza thamani ya mifugo yetu” alisema Dk Mhede.
Kuhusu utambuzi Dk Mhede alisema zoezi la chanjo ya mifugo linaenda sambamba na utambuzi ili kutenganisha mifugo iliyochanjwa na ambayo bado haijachanjwa na kudhibiti wizi wa mifugo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk Edwin Mhede (kushoto) akitoa chanjo ya mdondoo wa Kuku kama ishara ya kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo kwa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma Julai 21, 2025.
Alitoa wito kwa wataalamu wanaoenda kutekeleza kampeni hiyo kutumia na kuvitunza vifaa vya chanjo ili viwahudumie wafugaji kama ilivyokusudiwa.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Mwasiti Juma alisema chanjo hiyo itawainua wafugaji kiuchumi kutokana na kwamba sekta ya mifugo ni sehemu muhimu katika uchumi wa Kondoa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Shabani Millao amekiri kuipokea kampeni hiyo na kuahidi kuwasimamia wataalam wa chanjo na utambuzi wa mifugo kutekeleza kampeni hiyo kwa wafugaji wote wa wilaya hiyo.
Naye Daktari wa Mifugo Wilaya Kondoa ambaye ndiye Mratibu wa kampeni hiyo wilayani humo Dk Christian Mwiga alisema wilaya hiyo itachanja ng’ombe 200,000, mbuzi na kondoo 280,000 na kuku 460,000 huku akitoa wito kwa wafugaji kupeleka mifugo katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya chanjo.



