GGML yafanya jambo michezo sekondari Geita

GEITA; KAMPUNI ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) imejitosa kudhamini programu ya mashindano ya michezo kwa shule za sekondari, Halmashauri ya Manispaa ya Geita ili kukabiliana na tatizo la utoro.
Hatua hiyo imekuja kufuatia Manispaa ya Geita kuripoti changamoto ya mdondoko wa wanafunzi 2,547 wa shule za sekondari kipindi cha mwaka 2021 hadi 2023 kati yao wavulana 1,288 na wasichana 1,259.
Ofisa Elimu Sekondari Manispaa ya Geita, Rashid Muhaya alitoa taarifa hiyo Julai 22, 2025 katika hafla ya kufunga mashindano hayo yaliyofanyika viwanja vya shule ya sekondari ya wasichana Nyankumbu mjini Geita.

Muhaya amesema kwa mjibu wa takwimu za TSS, katika mwaka wa masomo 2021, mdondoko ulikuwa wanafunzi 916 kati yao wavulana 428, na wasichana wakiwa ni 488.
Amesema mwaka 2022, mdondoko ulikuwa wanafunzi 872, wavulana wakiwa 463 na wasichana 409, huku mwaka 2023 mdondoko ulikuwa wanafunzi 759 wavulana wakiwa 397 na wasichana 362.
Amesema GGML na Manispaa ya Geita wamelenga kuendelea kutumia mashindano hayo kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa elimu na kuhamasisha wanafunzi waendelee na masomo mpaka watakapohitimu.
Muhaya amesema kwa mwaka 2025 mashindano yalianza Julai 14 na kutamatika Julai 22, 2025 na kushirikisha shule za sekondari 40 ikiwemo shule za serikali 30 pamoja na shule 10 za taasisi binafsi.

Mwakilishi wa GGML, Elibariki Jambalu amesema GGML imeguswa kudhamini programu hiyo ili kufanikisha kampeni ya ‘Tukutane Shuleni, Tujenge Kesho iliyo Bora’ ili kusaidia watoto kutimiza ndoto zao.
“Kila kijana anayekatisha masomo, ni ndoto iliyovunjika, ni hasara kwa mustakabali wa Geita na jamii yote kwa ujumla, hii ndio sababu GGML iliona umuhimu wa kushiriki mashindano haya”, amesema Elibariki.

Mkurugenzi wa Halmashuri ya Manispaa ya Geita, Yefred Muyenzi amesema programu hiyo ni sehemu ya tiba ya tatizo la mdondoko wa wanafunzi ambapo jitihada zingine zinafanyika kumaliza tatizo.
Mkuu wa wilaya ya Geita, Hashimu Komba amepongeza programu hiyo na kuiagiza manispaa kuhakikisha inawashirikisha wazazi wawe sehemu ya mashindano kwa miaka ijayo ili kufikisha ujumbe kwa ufasaha.



