Mwanamke mbaroni tuhuma kuchinja watoto watatu wa mke mwenzake

WAKAZI wawili wa Mkoa wa Ruvuma wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhumu za mauaji, akiwemo Wende Luchagula (30) anayetuhumiwa kuwachinja watoto watatu wa mke mwenzake kwa sababu za wivu wa mapenzi.

Mtuhumiwa mwingine ni mkazi wa Kijiji cha Lihale, Leyson Mkinga (44) anayetuhumiwa kumuua Adamu Chengula (68) kwa kuvunja shingo na kumnyonga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chillya akizungumzia anayetuhumiwa kuua watoto, amesema Julai 12, 2025 saa 8:00 mchana katika Kijiji cha Milonji, Namtumbo, Wende alivizia mume wake na mama mzazi wa watoto hao ambaye ni mke mdogo wakiwa wameenda mnadani kisha kuwachinja watoto watatu.

Kati yao, wapo pacha Kulwa Lutelemula Samweli na Doto Lutelemula Samweli wenye umri wa miezi minane. Mwingine ni Lugola Samweli (6).

Alieleza kuwa mume wa mtuhumiwa huyo ameoa wake watatu lakini alikuwa akimpenda zaidi mke mdogo na watoto wake kitendo ambacho mtuhumiwa hakukipenda.

Inadaiwa alimvizia mume wake na mama mzazi wa watoto hao wakiwa wameenda mnadani kisha akatekeleza tukio hilo.

Alisema baada ya uchunguzi, Jeshi la Polisi lilikabidhi miili ya marehemu kwa familia kwa ajili ya taratibu za maziko na mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani.

Kuhusu mauaji ya Chengula, alisema Julai 7, 2025 saa 2:00 asubuhi katika Kijiji cha Lihale, Mbinga, Leyson akiwa na mwenzake Dastan Mkinga, mkazi wa Bombambili, mjukuu wa marehemu ambaye alikimbia baada ya kushirikiana kufanya tukio hilo walifika nyumbani kwa Chengula wakimtuhumu kuwa ni mchawi.

Kamanda Chillya alisema watuhumiwa hao baada ya kumuua Chengula walimuweka ndani ya zizi la mbuzi lililopo katika nyumba aliyokuwa akiishi (marehemu) na kutoroka kusikojulikana.

Alieleza kuwa baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilifanya msako na ilipofika Juni 24, 2025 saa 2:00 asubuhi Ruhuwiko, walimkamata Leyson hivyo wanaendelea kumtafuta Dastan ili wote wafikishwe mahakamani.

Habari Zifananazo

6 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button