Mizigo SGR neema kwa nchi

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limesema kusafirisha mizigo kwa Reli ya Kisasa (SGR) kuna manufaa makubwa kwa nchi.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano TRC, Fredy Mwanjala amelieleza gazeti la HabariLEO kuwa tangu walipoanza kusafirisha mizigo Juni 27, mwaka huu wanaifanya kazi hiyo kwa mafanikio.
“Katika kipindi hiki tunasafirisha mizigo ya makampuni makubwa na ya kati, makampuni ambayo tayari yanasafirisha mizigo na yaliyoonesha nia ni pamoja na Mikoani Traders (Azania Group of Companies), Mohamed Enterprises, kampuni za Saruji Dangote na Twiga,
pia Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP). Mizigo inayosafirishwa ni pamoja na bidhaa za ujenzi na matumizi ya binadamu,” alisema Mwajala.
Aliongeza: “Usafirishaji wa mizigo kwa SGR una faida kubwa kwa wateja wetu kwa kuokoa muda wa safari na kupunguza matumizi. Usafiri kati ya Dar es Salaam na Dodoma kwa lori ni takribani saa 12 wakati kwa SGR ni saa nne tu”.
Mwanjala alisema SGR inaokoa mabilioni ya Shilingi ambayo Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inatumia kukarabati barabara zinazoathiriwa na uzito wa malori.
“Pesa zinazookolewa zitaenda kutumika kuboresha zaidi maeneo kama ya afya, elimu na miundombinu,”alisema Mwanjala.
Alisema kwa sasa TRC inatumia magari kutoa mzigo Bandari ya Dar es Salaam kwenda kituo cha SGR Pugu na kisha inasafirishwa kwenda kituo cha SGR Ihumwa mkoani Dodoma.
“Treni ya zamani MGR yenyewe inatoa mzigo moja kwa moja Bandari ya Dar es Salaam kupeleka bandari kavu ya Kwala wakati huu. Mradi wa Port Link unaendelea kutekelezwa na utakapokamilika SGR nayo itaanza kuchukua mzigo bandarini na kuupeleka moja kwa moja bandari kavu ya Kwala,” alifafanua.
Hivi karibuni, Mwanjala alipozungumza na Kituo cha Televisheni cha UTV cha Kampuni ya Azam Media alisema TRC ipo katika mchakato wa kukamilisha taratibu za kushirikisha sekta binafsi katika usafirishaji wa abiria na mizigo kwa kutumia SGR.
Alisema taratibu zitakapokamilika serikali itazialika taasisi na sekta binafsi kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo kupitia treni ya SGR.
Mwanjala alisema serikali imefanya marekebisho ya Sheria ya TRC ili kuruhusu sekta binafsi kushiriki katika usafirishaji wa mizigo na abiria kupitia reli ya kisasa.
“Sheria iliyounda Shirika la Reli Sheria Namba 10 ya 2017 ilifanyiwa marekebisho 2023 ili kuruhusu sekta binafsi kushiriki katika usafirishaji kwenye reli. Kinachoendelea sasa kwa TRC ni kukamilisha taratibu kushirikisha sekta binafsi kukiwa na ushindani wenye haki,” alieleza Mwanjala.
Mwanjala alisema shirika hilo lina miundombinu ya reli ya kisasa, mabehewa na vichwa vitakavyoweza kutumiwa na sekta binafsi kuwekeza katika usafirishaji wa mizigo na abiria na tayari kanuni zimeshatungwa kuwezesha ushirikiano huo.
Alisema kampuni nyingi zinazomilikiwa na sekta binafsi zimeonesha mwitikio chanya kwa kuitikia kwa wingi kusafirisha mizigo kupitia SGR.
Mwanjala alisema TRC ina mabehewa ya kutosha ya kusafirisha mizigo kwa kuwa na mabehewa 264 yakiwamo 200 ya kubeba makasha, na pia inajipanga kufunga mabehewa mengine 30 yenye uwezo wa kubeba tani 2,100 kwa wakati mmoja.
Alisema wanaendelea na ujenzi wa kipande cha SGR kutoka bandarini ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo moja kwa moja kutoka Bandari ya Dar es Salaam na ujenzi upo katika hatua nzuri.
Kuhusu mafanikio kiutendaji, alisema katika kipindi cha majaribio ya treni hiyo imefanikiwa kiufundi na kiuendeshaji kwani katika safari zake zote mbili imepakia, kushusha na kusafirisha mizigo sawasawa na kutumia muda wa safari uliopangwa.
Hivi karibuni, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema SGR ya mizigo itasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa bandari na kuokoa uharibifu wa barabara kuchochea ajira kwa wakazi wanaozunguka
Bandari kavu ya Kwala.
Pia, Profesa Mbarawa alisema usafirishaji kupitia reli hiyo utapunguza muda uliokuwa unatumika kusafirisha mizigo kwa malori na kutoa uhakika wa safari na kuondoa vihatarishi vya usafirishaji wa mizigo yao.
“Usafirishaji wa mizigo kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa magari ya mizigo yanatumia masaa 12, lakini kwa upande wa reli ya kisasa ya SGR mzigo utasafirishwa kwa masaa manne tu haya ni maendeleo makubwa,” alisema Profesa Mbarawa.
Alisema safari ya kwanza Juni 27, 2025 kwa treni hiyo ilianza na kusafirisha makasha 10 yenye tani 700 za bidhaa mchanganyiko huku safari ya pili ilifanyika Julai 9, 2025 na kusafirisha makasha 20 yenye tani 1,400 na itaendelea kuongeza idadi ya makasha.
Awali, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa alisema SGR itakuwa na manufaa zaidi kiuchumi kwa kusafirisha mizigo na si abiria.
“Unajua treni ni mizigo, abiria haturudishi gharama kwa asilimia 100, sisi akili yetu ipo kwenye mizigo zaidi kuliko kwenye abiria, abiria ni huduma, pesa yetu ipo kwenye mizigo. Tunajenga reli ya kwenda Msongati, pale Msongati kuna machimbo yale ya Nickel,” alisema Kadogosa.
Aliongeza: “Msongati tunaenda kwa sababu tutapata mzigo na yale machimbo yanakadiriwa yanaweza yakaenda miaka 100 yaani kuanzia miaka 50 kwenda mbele. Tunasomba mzigo maana yake kutoa kule kupeleka, kama watakuwa wanachimba ni China tutakuwa tunapeleka China, lakini kupitia kwenye bandari”.
Bandari kavu ya Kwala Profesa Mbarawa alisema kukamilika kwa bandari kavu ya Kwala kutaongeza ufanisi kutokana na ongezeko la shehena inayohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam.
“Kutakuwa na ongezeko la mapato ya serikali kupitia huduma zitakazotolewa na kupunguza gharama za uendeshaji na kuvutia wafanyabiashara kutumia bandari yetu ya Dar es Salaam na kuimarisha uchumi wetu,”
alisema.
Aidha, alisema bandari hiyo itapunguza msongamano wa magari na kuimarisha shughuli za biashara na uchumi kwa wananchi.
Alisema kabla ya kujengwa bandari hiyo kulikuwa na msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam ukiwamo wa meli.
Pia, Profesa Mbarawa alisema bandari kavu ya Kwala ilijengwa kutokana na uwezo mdogo wa bandari kavu zilizokuwepo awali.
“Dar es Salaam tulikuwa na bandari kavu 11 zenye uwezo wa kuhifadhi makasha 24,300 kwa wakati mmoja na bandari kavu za kuhifadhia magari tisa zenye uwezo wa kuhifadhia magari 19,100 tu kwa wakati mmoja ambazo zilionekana kutokidhi mahitaji makubwa,” alifafanua.
Profesa Mbarawa alisema kwa sasa bandari hiyo itahudumia makasha 823 kwa siku na kupunguza asilimia 30 ya makasha yanayohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam.
Alisema jiografia ya Kwala inawezesha eneo hilo kuunganishwa kirahisi na barabara ya Chalinze – Dar es Salaam inayounganisha barabara zinazoenda nchi jirani.
Keshokutwa Alhamisi, Rais Samia Suluhu Hassan atazindua Bandari kavu ya Kwala, reli ya mizigo ya SGR na mabehewa 50 mapya na mengine 20 yaliyokarabatiwa kwa hisani ya Wakala ya Ushoroba wa Kati.



