Tuzidishe juhudi kuvutia wawekezaji sekta ya makazi
KWA mujibu wa takwimu za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa sasa kuna uhitaji wa makazi milioni 3.8 nchini kwa mwaka kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kukua kwa miji.
Kwa mujibu wa waziri wa wizara hiyo, Deogratius Ndejembi, miaka ya 1960 na 1967 ukuaji katika miji ulikuwa katika asilimia 6.2 tu, lakini katika Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ukuaji wa miji umekwenda asilimia 34.9.
Ndejembi anasema tayari serikali imechukua hatua mbalimbali, ikiwamo uzinduzi wa Sera ya Ardhi ya 1995 Toleo la 2025 inayoruhusu uwekezaji katika sekta ya makazi ili kukabiliana na changamoto hiyo na kuhakikisha wananchi wanapata makazi kwa bei nafuu.
Mbali na hilo, pia serikali imeandaa mipango mbalimbali ikiwamo nyumba za bei nafuu za Samia ambazo mwananchi atanunua kwa bei nafuu pamoja na kuendelea na mazungumzo na mataifa mengine kwa ajili ya kupata teknolojia mpya katika ujenzi wa makazi na kuendeleza miji na majiji nchini.
Ndiyo maana katika eneo hilo, Ndejembi amewataka wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta ya makazi nchini kwa sababu kuna uhitaji mkubwa.
Tunaungana na waziri katika kuwaomba wawekezaji wa ndani na nje kuona namna ambavyo watatumia mipango hii ya serikali kuwekeza katika sekta ya makazi.
Sote tunafahamu kuwa makazi mazuri ni kielelezo mojawapo cha kukua kwa uchumi, hivyo miji yetu inapokuwa na makazi mazuri maana yake inachangia katika maendeleo ya nchi na kuifanya pia sekta ikue kwa haraka.
Tumeshuhudia si tu ukosefu wa makazi bora nchini, bali bado kuna maeneo katika miji nchini yana makazi duni, hali ambayo inazorotesha ustawi wa wananchi kwa kukaribisha pia matatizo mengine yakiwamo ya maradhi.
Kwa msingi huo, tunaamini serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta hii muhimu kwa maendeleo ya uchumi, kama ambavyo tumeshuhudia wiki hii wawekezaji kutoka Japan wapo nchini kuona fursa katika sekta hii.
Japan ni moja ya nchi zilizopiga hatua kubwa katika sekta ya makazi, na Tanzania imepata uwekezaji kutoka nchi hiyo katika sekta za viwanda, nyumba na miundombinu.
Tuitumie Japan kama moja ya nchi ambazo wawekezaji watavutiwa kuendelea kuja kuwekeza nchini katika sekta ya makazi, hasa kutokana na ukweli kwamba imepiga hatua kubwa katika eneo hilo baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia na sasa takwimu zinaonesha kuwa kuna ziada ya makazi milioni nane katika nchi hiyo ya Asia.



