Msanii Davina kugombea ubunge viti maalum kupitia NGOs

IRINGA: Kada wa CCM na msanii maarufu wa filamu nchini, Halima Yahaya Mpinge ‘Davina’, ameonesha shukrani zake kwa Chama Cha Mapinduzi kwa kumteua kuwa mgombea wa Ubunge wa Viti Maalum kupitia kundi la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs).
Akizungumzia uchaguzi huo utakaofanyika mjini Dodoma, jumamosi ijayo, Davina amesema:
“Nashukuru sana chama changu kipenzi CCM kwa kuniamini na kuniteua kuwa mgombea wa nafasi hii muhimu. Naomba kura zenu ndugu zangu, hasa wajumbe, ili tuweze kushinda na kuendelea kuwahudumia wananchi.”
Amesema hili ni jaribio lake la pili kwake baada ya kuwania nafasi hiyo mwaka 2020 lakini kukosa kura za kutosha.

“Leo nimerudi kwa nguvu mpya na ari mpya,” amesema Davina.
Kwa sasa, Davina ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa na Maadili ya Wilaya ya Iringa Vijijini na pia Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT Mkoa wa Iringa.
Ameahidi kuwa sauti ya wanawake na vijana bungeni, endapo atapata nafasi hiyo, akiahidi kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza maendeleo ya taifa.


