Ngajilo Iringa Mjini: “Niko tayari kwa majukumu”

IRINGA: Fadhili Fabian Ngajilo ameishukuru Kamati Kuu ya CCM Taifa kwa kumteua kuwa mmoja wa wagombea katika mchakato wa kura za maoni kuwania ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini, akisema uteuzi huo ni heshima kubwa kwake na ushahidi wa imani ya chama juu ya uwezo wake wa kiuongozi.
“Ninajivunia kuwa sehemu ya wana-CCM waliopata nafasi hii adhimu. Nitashiriki mchakato huu kwa heshima, uadilifu na kwa dhamira ya kweli ya kulitumikia jimbo langu,” amesema Ngajilo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Iringa.
Ngajilo amesema uzoefu alioupata ndani ya chama kwa zaidi ya miaka 20 na katika taaluma ya ualimu wa vyuo vikuu unampa ujasiri wa kusimamia maendeleo ya Iringa Mjini kwa vitendo.
Pamoja na Ngajilo wengine walioteuliwa na Kamati Kuu kushiriki mchakato huo wa awali ni pamoja na Jesca Msambatavangu (mbunge anayemaliza awamu ya kwanza), Mch. Peter Msigwa, Wakili Moses Ambindilwe, Islam Huwel na Nguvu Chengula.
Ngajilo amesema endapo atapata ridhaa ya wajumbe, atatoa kipaumbele kwa fursa za kiuchumi, uwajibikaji wa viongozi na huduma bora za kijamii.

