Mradi wa urani ni dira ya uchumi

RUVUMA: RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa kukamilika kwa kiwanda cha majaribio cha uchenjuaji wa madini ya urani kilichopo wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma ni hatua ya kimkakati itakayoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji 10 wakuu wa urani duniani rasilimali muhimu katika uzalishaji wa nishati safi.
Akizungumza mbele ya wananchi mara baada ya kuzindua rasmi kiwanda hicho, Rais Samia amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya serikali kuifikisha Tanzania katika uchumi wa viwanda unaojitegemea, huku akisisitiza kuwa kila hatua ya utekelezaji itazingatia viwango vya kimataifa, usalama wa afya na mazingira.
Ameeleza kuwa tayari ameshuhudia kwa macho mitambo ya uchenjuaji wa madini hayo na kupongeza namna mwekezaji alivyojipanga kuongeza thamani ya rasilimali hiyo ndani ya nchi.
Kwa mujibu wa Rais Samia, mradi huo wa Mto Mkuju unatarajiwa kudumu kwa zaidi ya miaka 20 ya uzalishaji na katika kipindi hicho, Tanzania itanufaika kwa uwekezaji wa takriban dola za Marekani bilioni 1.2 ambayo ni sawa na zaidi ya Sh trilioni 3.2, ajira za muda mfupi zipatazo 3,500 hadi 4,000 wakati wa ujenzi wa miundombinu, ajira za moja kwa moja za kudumu zipatazo 750, na ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 4,500 kutokana na shughuli zitakazochochewa na uwepo wa mradi huo.



