Melabu kukomalia barabara, kiwanda cha chai Mufindi Kaskazini

Mtia nia ubunge Jimbo la Mufindi Kaskazini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Luqman Melabu, ameahidi kutumia ujuzi na uzoefu alionao kupitia kampuni yake ya ujenzi kushirikiana na serikali kumaliza changamoto ya barabara sugu jimboni humo, sambamba na kusogeza huduma muhimu kwa wananchi, hususani kaya masikini.

Akizungumza kwenye mikutano ya kuomba kura kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, Melabu alisema moja ya changamoto kubwa inayowanyima wananchi fursa ya kustawi kiuchumi ni ubovu wa barabara, hasa kipindi cha mvua ambapo wakulima hushindwa kusafirisha mazao yao kwa wakati na hivyo kuuza kwa bei ya hasara.

“Changamoto hizi mimi nazielewa kwa undani kwa sababu mimi ni mkazi wa Mufindi Kaskazini na ninaishi kijijini Lulanda. Kwa nafasi niliyonayo, nitatumia kampuni yangu kushirikiana na serikali kuhakikisha barabara zinajengwa kwa viwango vya kudumu na kukarabatiwa ili zipitike mwaka mzima. Nipeni ridhaa, nitautumia ujuzi huu kuhakikisha Mufindi Kaskazini inasonga mbele,” alisema Melabu.

Mbali na barabara, Melabu ameweka kipaumbele katika huduma za umeme kwa vitongoji vyote ambavyo bado havijafikiwa, akisisitiza kuwa ataweka mkakati wa kusaidia kaya masikini kwa kuzibebea gharama za nguzo za umeme.

“Umeme lazima uifikie kila kaya ifikapo mwaka 2030. Sitakubali familia zetu zikwame kwa sababu ya gharama za nguzo. Nitazisaidia kaya masikini kupata nguzo bure, ili maendeleo ya vijiji vyetu yawe jumuishi na ya haraka,” aliongeza.

Kwa mujibu wa Melabu, ukarabati wa barabara na upatikanaji wa umeme vitakuwa injini kuu za kusukuma maendeleo mapya Mufindi Kaskazini kwa kurahisisha usafirishaji wa mazao, kupanua fursa za biashara na kuongeza ajira kwa vijana.

“Maendeleo ya Mufindi Kaskazini hayawezi kusubiri. Tunahitaji barabara bora, umeme kwa kila kaya na huduma za afya nafuu. Hayo ndiyo mapambano yangu kwa kushirikiana na serikali na ninyi wananchi,” alisisitiza.

Melabu pia ameahidi kupigania kufunguliwa kwa Kiwanda cha Chai cha Itona au kusaka mwekezaji mpya, sambamba na kutumia mtandao wake wa kibiashara kuvutia wawekezaji kujenga viwanda katika kata zote za jimbo hilo ili kuongeza ajira kwa vijana.

Mbali na Melabu, wanaowania tiketi ya CCM kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu ni pamoja na mbunge anayemaliza muda wake Exaud Kigahe, Prof. Obadia Nyongole, Alban Lutambi na Godfrey Ngupula.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button