Vyombo vya habari vyatakiwa kufuata sheria,kanuni za uchaguzi

DAR ES SALAAM :MWENYEKITI wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele, amewataka wanahabari kote nchini kutumia taaluma yao kwa weledi katika kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ili kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu kwa amani na utulivu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kitaifa kati ya INEC na waandishi wa habari ulioandaliwa kwa lengo la kuwaandaa vyema wanahabari kuelekea uchaguzi huo, Jaji Mwambegele amesema ni muhimu vyombo vya habari kuwa chanzo cha maarifa sahihi na yenye kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika mchakato wa kidemokrasia.

“Tunahitaji wanahabari kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha wananchi juu ya mchakato wa uchaguzi. Habari zenu zinaweza kuwa chachu ya wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa Oktoba kwa amani na utulivu,” alisema Jaji Mwambegele.

Ameongeza kuwa uchaguzi wa mwaka huu utahusisha majimbo 272 ya uchaguzi, hivyo ni muhimu kwa wanahabari waliopewa mafunzo na tume kuhakikisha wanazingatia maadili, kanuni na sheria za uchaguzi. SOMA: Mwenyekiti INEC aeleza waratibu waliyojifunza kuelekea uchaguzi

Aidha, baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki mkutano huo akiwemo Upendo Media, Luseshelo Sijaona na Bahati Alex, wameipongeza INEC kwa kubuni mfumo wa kugawa makundi ya wanahabari kwa ajili ya mafunzo, wakieleza kuwa hatua hiyo itawawezesha kuripoti kwa ufanisi na kutoa habari zenye weledi na tija kwa jamii.“Kwa namna hii, tunaamini tutaweza kuwafikia wananchi wengi kwa habari zilizo sahihi, kwa wakati na kwa kuzingatia misingi ya kitaaluma,” alisema Luseshelo.

Mkutano huo ni miongoni mwa mikakati ya INEC kuhakikisha wadau wa habari wanashiriki kikamilifu katika kufanikisha uchaguzi huru, haki na wa amani.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button