Mbio nishati safi zafana Arusha

ARUSHA: Mbio za Nishati Safi ya Kupikia zimemalizika jijini Arusha zikiwa na lengo la kuhamasisha, kutoa elimu na mafunzo juu ya matumizi ya nishati salama.
Mbio hizo zimehusisha washiriki 350 kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Arusha washindi watano katika mbio za km 21,km10 na km 5 walikabidhiwa zawadi za majiko ya gesi pamoja na umeme.
Mwandaaji wa mbio hizo Noureen Mawalla kutoka Tabwa amesema Kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia itaendeshwa katika kanda tano na sasa imemalizika kanda ya.Kaskazini kwa watu 350 kushiriki na sasa itafanyika Kanda ya Ziwa na kanda ya kati.

“Mwitikio ni mkubwa watu wanaweza kujifunza na kupata uelewa kwani awali walikuwa hawaelewi ila sas tunaona mwamko mkubwa katika matumizi ya nishati safi na hii ni kutokana na elimu inayoendelea kutolewa,”alisema Mawalla.
Ameongeza kuwa matarajio yao ni kuendelea kuhamasisha kupitia michezo kwa maana ya mbio na aliwashukuru wote waliohusika kufanikisha .
Akizungumza katika mbio hizo Mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa Nishati safi ya kupikia kutoka Wizara ya nishati Nolasco Mlay amesema wao kama serikali wanaendelea kutoa mkato na msisito katika matumizi sahihi ya Nishati hii salama.
Alisema kwa mujibu wa takwimu watu 33,000 kila mwaka wanakufa kutokana na nishati isiyo salama hivyo ni wajibu wetu kuendelea kutumia nishati safi kwa kutoa elimu kote.

“Rais wetu ndio kinara wa kampeni hii ya matumizi ya Nishati safi kwani itatusaidia kuhakikisha tunalinda afya na mazingira yetu na kama Wizara malengo yetu ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 tuwe tanatumia nishati safi,”alisema Mlay.
Naye Ofisa Michezo wa jiji la Arusha Benson Maneno amesema kama serikali inatoa shukrani kwa waandaaji kutokana na kutumia vitu vya maendeleo katika kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa nishati safi.



