THRDC yaipongeza CCM uteuzi makundi maalumu

DAR ES SALAAM: Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umetoa wito kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhakikisha uteuzi wa wawakilishi wa makundi maalum ndani ya Bunge, hasa Asasi za Kiraia (NGOs) na watu wenye mahitaji maalum, unafanyika kwa kutumia vigezo mahsusi na si kushirikisha wajumbe wote wa chama katika mchakato huo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 4, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, amesema hatua hiyo itasaidia kupata wagombea wenye sifa, weledi na uzoefu wa kufanya kazi na jamii kupitia NGOs, tofauti na hali ilivyo sasa ambapo yeyote anaweza kuomba na hata kupitishwa bila kuwa na uhusiano wa karibu na sekta hiyo.

“Tunakipongeza Chama cha Mapinduzi kwa hatua ya kujumuisha uwakilishi wa NGOs kupitia Ilani yake ya Uchaguzi. Hii ni hatua chanya na ya mfano kwa vyama vingine vya siasa ambavyo bado havajatambua umuhimu wa sauti ya asasi za kiraia bungeni,” amesema Olengurumwa.

SOMA ZAIDI

CCM masikio Kamati Kuu leo uteuzi

Hata hivyo, ameongeza kuwa licha ya hatua hiyo kuwa ya kupongezwa, bado kuna changamoto katika mchakato wa uteuzi, hususan ukosefu wa vigezo vinavyotambua kwa uwazi sifa na historia ya wagombea wanaowakilisha NGOs. Ameeleza kuwa hali hiyo huongeza uwezekano wa kuchaguliwa kwa watu wasiokuwa na uzoefu wala uelewa wa sekta hiyo nyeti.

“Wengi wa wapiga kura hawana maarifa ya kutosha kuhusu mchango na kazi ya NGOs, hivyo huweza kumpitisha mgombea yeyote, hata kama hajawahi kushiriki kwenye shughuli zozote za kiraia. Hii ni hatari kwa mustakabali wa uwakilishi wa asasi hizi,” amefafanua.

Olengurumwa amependekeza nafasi hiyo kutolewa kwa watu waliowahi au wanaoendelea kufanya kazi ndani ya NGOs, badala ya wafanyabiashara au watu wengine wasiohusika moja kwa moja na sekta hiyo. Amesisitiza pia umuhimu wa kufanyika kwa maboresho ya sheria ili kuhakikisha kuwa wapiga kura wanaoshiriki kuchagua wawakilishi wa NGOs wanatoka ndani ya asasi hizo wenyewe.

THRDC imeendelea kuwa mstari wa mbele kutetea nafasi ya asasi za kiraia katika mchakato wa maamuzi ya kitaifa, ikisisitiza kuwa ushiriki wa makundi hayo ni nyenzo muhimu ya kukuza demokrasia na uwajibikaji katika jamii.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button