Tanzania, Qatar zakubaliana vyeti vya mabaharia

LONDON; Serikali ya Tanzania na Serikali ya Qatar zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) ya kutambuliana vyeti vya mabaharia katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika jijini London.

Hafla hiyo imefanyika pembezoni mwa mkutano wa 34 wa Baraza Kuu la Shirika la Bahari Duniani na kuhudhuriwa na viongozi pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya bahari.

Kwa upande wa Tanzania, makubaliano hayo yamesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mohamed Malick Salum, huku Mhandisi Abdulaziz Abdullah Al-Sulait, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi wa Qatar, akisaini kwa niaba ya nchi yake.

Kupitia MoU hiyo, pande zote mbili zinatarajia kuboresha viwango vya umahiri, usalama na ubora katika taaluma ya ubaharia, sambamba na kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Qatar.

Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ajira kwa mabaharia wa Kitanzania katika meli zilizosajiliwa au kuendeshwa na kampuni za Qatar, kwani hawatalazimika kupitia upya taratibu za uthibitishaji wa vyeti pamoja na kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafirishaji baharini kati ya nchi hizo mbili.

Aidha makubaliano haya yatawezesha mabaharia kupata maslahi bora na fursa zaidi za kazi kwenye masoko yenye ushindani wa juu na kunachochea uhamishaji wa ujuzi na utaalamu wa kimataifa.

Hatua hiyo itasaidia kwa kuwa mabaharia watafanya kazi katika majukwaa yenye viwango vya juu vya teknolojia na usalama pamoja na kuimarisha uwezo wa Tanzania katika utoaji wa mafunzo ya ubaharia, kwani vyuo na vyeti vyake vitakuwa na uhalali mpana zaidi kimataifa.-

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button