Kusiluka: Tuache kazi kwa mazoea Dira 2050

SERIKALI imeagiza viongozi waache kufanya kazi kwa mazoea.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka alisema hayo katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha jana akifungua kikaokazi cha makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wote kwa ajili ya kujadili utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Rais Samia Suluhu Hassan alizindua dira hiyo Julai 17, mwaka huu.

Dk Kusiluka alisema huu si wakati wa kuendelea na kazi kwa mazoea kwani kupitia LTPP hiyo, Tanzania inatarajiwa kufikia malengo ya Dira 2050 likiwemo la kuwa na Pato la Taifa (GDP) la Dola trilioni moja za Marekani ifikapo mwaka 2050.

Aliwataka washiriki waifahamu na kuelewa Dira 2050 na maudhui ya Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu (LTPP) na wachangie kwa dhati ili kuandaa LTPP inayotekelezeka na halisia.

Dk Kusiluka alisema makatibu wakuu wanapaswa kutoa mchango usioishia katika wizara zao kwa kuwa huwa wanabadilishana wizara mara kwa mara.

Awali, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Tausi Kida alimshukuru Katibu Mkuu Kiongozi kwa kuchukua muda wake kushiriki kikao hicho muhimu kwa utekelezaji wa Dira 2050 katika kupitia maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu wa miaka 25, muda wa kati na mfupi ya miaka mitano na mmoja, mtawalia.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dk Fred Msemwa aliwakumbusha maagizo yaliyotolewa na Rais Samia wakati wa uzinduzi wa Dira 2050 kuwa yazingatiwe wakati wa utekelezaji.

Dk Msemwa alitaja maagizo hayo kuwa ni pamoja na mabadiliko ya mtazamo katika utendaji kazi, kila wizara kufanya uhakiki wa sera zilizopo kama zinaendana na Dira 2050 na kufanyia marekebisho sheria ili ziendane.

Maagizo mengine ni kushirikisha sekta binafsi kama mhimili mkuu, kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini, pamoja na kuendesha kampeni ya uelimishaji wa umma ili kila Mtanzania aelewe maudhui ya Dira 2050.

Kikaokazi hicho kiliandaliwa na Tume ya Taifa ya Mipango ikiwa ni hatua za awali za utekelezaji wa dira kwa lengo la kupata maoni ya makatibu wakuu katika uandaaji wa Mpango wa Maendeleo wa muda mrefu wa miaka 25 na mipango ya kati na mfupi ya miaka mitano na mwaka mmoja, mtawalia.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyewakilishwa na Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole, wajumbe wa kikosikazi cha kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu wakiongozwa na Balozi Dk Asha-Rose Migiro na watumishi na menejimenti ya Tume ya Taifa ya Mipango.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button