Ndejembi azindua kituo cha kuchajia magari

SERIKALI imezindua Kituo cha Kuchajia Vyombo vya Usafiri Vinavyotumia Umeme jijini Dodoma, katika hatua inayolenga kuharakisha matumizi ya nishati safi na kupunguza gharama za usafiri nchini.

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, alizindua kituo hicho katika Ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), akisema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika sekta ya usafirishaji na matumizi ya majumbani.

Uzinduzi huo uliambatana na utiaji saini wa miradi mbalimbali ya nishati safi, ikiwemo Mradi wa Ujenzi wa Vituo vya Kuchajia Vyombo vya Usafiri Vinavyotumia Umeme (EV Charging Stations) na Mpango wa Ukopeshaji wa Majiko ya Umeme kwa Wateja wa TANESCO kupitia mfumo wa On-Bill Financing (OBF).

Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika Viwanja vya Mashujaa, Jamatini jijini Dodoma, Ndejembi alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha Watanzania wanapata nishati safi, nafuu na yenye ufanisi kwa matumizi ya kila siku.“Miradi hii ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kuongeza upatikanaji wa huduma za umeme katika sekta mbalimbali za uchumi,” alisema Ndejembi.

Kwa mujibu wa TANESCO, vituo vya kuchajia magari ya umeme vinatarajiwa kusaidia kuongezeka kwa matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme nchini, sambamba na kupunguza matumizi ya mafuta ya petroli na dizeli.

Aidha, mpango wa ukopeshaji wa majiko ya umeme unalenga kuwawezesha wananchi kupata vifaa vya kupikia vinavyotumia umeme kwa urahisi zaidi, hatua inayotarajiwa kuchangia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia.

Serikali inaamini kuwa uwekezaji katika teknolojia za nishati safi utasaidia kupunguza gharama za nishati, kulinda mazingira na kuchochea maendeleo ya uchumi wa kijani nchini.SOMA: Tanesco yapewa siku 7 kufikisha umeme bweni la Shishiyu

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button