Shule binafsi zataka mazingira rafiki kuelekea 2028

WAKATI Tanzania ikiendelea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, wadau wa elimu wameonya kuwa mafanikio ya sekta hiyo hayatapatikana kwa juhudi za serikali pekee, bali kwa ushirikiano wa dhati kati ya serikali na sekta binafsi ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikibeba sehemu muhimu ya jukumu la kutoa elimu kwa Watanzania.
Wito huo umetolewa katika mkutano wa Umoja wa Wamiliki wa Shule Binafsi Tanzania (TAMONGSCO) uliofanyika mkoani Iringa, ambapo viongozi wa shule binafsi walieleza changamoto mbalimbali zinazohatarisha uwekezaji katika elimu huku wakitaka kuwepo kwa mazingira yanayochochea ushirikiano badala ya migongano.
Kaimu Mwenyekiti wa TAMONGSCO Kanda ya Nyasa, Dk Yahaya Msigwa, amesema shule binafsi zinaendelea kukabiliana na changamoto za kodi, pamoja na taratibu ambazo wakati mwingine huonekana kuwaadhibu badala ya kuwajengea uwezo.
Amesema pamoja na wawekezaji wa elimu kuwekeza fedha nyingi katika ujenzi wa madarasa, mabweni, maabara na ajira za walimu, bado wanahitaji kutambuliwa kama washirika wa maendeleo badala ya kuonekana kama wapinzani wa serikali.
“Tunachoomba ni ushirikiano wa kweli. Sisi si maadui wa serikali, bali ni wadau wanaosaidia kutekeleza jukumu la kuelimisha watoto wa Tanzania. Mazingira bora ya uwekezaji yataongeza uwezo wetu wa kutoa elimu bora zaidi,” alisema Dk Msigwa.

Mbali na changamoto za kodi, alieleza kuwepo kwa malalamiko ya muda mrefu kuhusu baadhi ya wanafunzi kutoka shule binafsi kukosa nafasi katika shule za vipaji maalumu licha ya kufanya vizuri kitaaluma, jambo ambalo limekuwa likizua maswali kuhusu usawa wa fursa katika mfumo wa elimu.
Hata hivyo, serikali imesema inaendelea kuthamini mchango wa sekta binafsi na kwamba ushirikiano huo unakuwa muhimu zaidi wakati nchi ikiandaa mapokezi ya ongezeko kubwa la wanafunzi wanaotarajiwa kuingia sekondari mwaka 2028.
Akizungumza kwa niaba ya Ofisa Elimu Mkoa wa Iringa, Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Iringa, Reginaldo Msende, alisema mabadiliko ya mtaala yaliyoboreshwa yatasababisha mwaka 2027 kuwa na wanafunzi wa makundi mawili watakaohitimu elimu ya msingi kwa wakati mmoja.
Alifafanua kuwa kuanzia mwaka 2027 wanafunzi watahitimu elimu ya msingi wakiwa darasa la sita, hivyo mwaka 2028 kutakuwa na wanafunzi wa darasa la sita na darasa la saba watakaojiunga na elimu ya sekondari kwa pamoja.
“Serikali iliona hali hii mapema na ndiyo sababu maandalizi yalianza kwa wakati. Tumejenga shule mpya za sekondari katika awamu mbalimbali nchini kote ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekosa nafasi ya kuendelea na elimu,” alisema Msende.

Alieleza kuwa serikali imejenga shule maalumu za wasichana katika mikoa yote 26 ya Tanzania pamoja na shule za wavulana za kikanda ili kuongeza uwezo wa kupokea wanafunzi wengi zaidi.
Kwa Mkoa wa Iringa, alitaja uwepo wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Lugalo iliyopo Wilaya ya Kilolo kama sehemu ya uwekezaji mkubwa unaolenga kupanua fursa za elimu kwa watoto wa kike.
Mbali na miundombinu, Msende alisema serikali inaendelea kusukuma mbele utekelezaji wa elimu ya amali ili kuhakikisha wahitimu wanapata maarifa na ujuzi unaowawezesha kujitegemea badala ya kutegemea ajira pekee.
Alisisitiza kuwa mafanikio ya mabadiliko hayo yatategemea ushirikiano wa karibu kati ya serikali, wamiliki wa shule, walimu na wazazi katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora yenye kuzingatia maarifa, maadili na stadi za maisha.
Wadau wa elimu wanaamini kuwa mwaka 2028 utakuwa mtihani mkubwa kwa mfumo wa elimu nchini, lakini pia ni fursa ya kuonesha jinsi ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi unavyoweza kutatua changamoto za maendeleo.
Mkutano huo umeacha ujumbe mmoja muhimu; kwamba mustakabali wa elimu ya Tanzania haujengwi kwa mgawanyiko, bali kwa uwajibikaji, ushirikiano na maamuzi yanayomweka mwanafunzi katikati ya kila sera na uwekezaji unaofanywa.



