Gharama za maji Kigoma Ujiji zapanda

KIGOMA: MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma Ujiji (KUWASA) imefanya mabadiliko ya gharama ya bei za maji kwa wateja wake.
Akitangaza mabadiliko hayo leo Juni 9, Ofisa Mipango na Uchumi wa KUWASA, Naaman Kahoye kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Dk. Christopher Nditi amesema bei za huduma ya maji kwa wateja wa majumbani zimepanda kutoka Sh 1415 kwa unit moja za awali na bei mpya kufikia 1850.
Kahoye amesema kwa wateja wa taasisi gharama imepanda kutoka Sh 1700 inayotumika kwa sasa na kufikia Sh 2253, wateja wa biashara na viwanda bei imepanda kutoka Sh 1800 na kufikia Sh 2385.
Akizungumza katika mkutano huo wa kutangaza bei mpya Mkurugenzi Mtendaji wa KUWASA, Dk.Chiristopher Nditi amesema mamlaka hiyo imekumbwa na changamoto kubwa kutokana na mapato kutokidhi hali halisi ya uendeshaji jambo linalowafanya kuongeza bei ya maji.




