Niliteswa na aibu ya picha mtandaoni

DAR-ES-SALAAM : MUIMBAJI na muigizaji maarufu nchini, Lulu Abas, anayefahamika zaidi kwa jina la kisanii Lulu Diva, amefunguka kwa mara ya kwanza kuhusu tukio la kusikitisha lililomkumba miaka kadhaa iliyopita kwa kusambazwa kwa picha zake za utupu kwenye mitandao ya kijamii.

Akizungumza katika mahojiano maalum na kipindi cha Leo Tena kinachorushwa na Clouds FM, Lulu alieleza kuwa picha hizo zilivuja mtandaoni baada ya kuachana na mpenzi wake wa zamani, raia wa Uingereza mwenye umri wa zaidi ya miaka 50. “Nilijua vijana wameshaniumiza sana, nikasema nijitulize kwa mtu mzima, kumbe naye ana matatizo ya kisaikolojia,” alisema Lulu kwa sauti ya kujiamini lakini iliyojaa huzuni.

Ameeleza kuwa picha hizo zilitokana na mawasiliano yao ya karibu kupitia simu wakati wa uhusiano wao, ambapo mara nyingine walizungumza hata wakati akiwa bafuni. Hata hivyo, hali ilibadilika walipoachana, ndipo mwanaume huyo alipoamua kuzisambaza kama njia ya kulipiza kisasi. “Picha zilivujishwa baada ya mimi kumkataa, ilinitesa hadi nikanywa sumu,” alisimulia kwa uchungu.

SOMA: Wanawake Sudan njiapanda udhalilishaji kingono

Kwa sasa, Lulu ameamua kuligeuza tukio hilo kuwa somo kwa jamii, hasa kwa vijana wanaoingia kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa njia ya kidigitali. “Kamwe usiruhusu kupigwa picha za utupu au kuzituma kwa mpenzi wako, hata kama unampenda kiasi gani. Teknolojia inabadilika, lakini aibu ya picha hizo kusambaa haifutiki kirahisi,” aliongeza.

Kauli ya Lulu imeibua mjadala mpana kuhusu usalama wa faragha katika mahusiano ya kimapenzi, hususan yale ya mtandaoni. Wadau wa teknolojia na wanaharakati wa haki za wanawake wameshauri kuwepo kwa elimu ya matumizi salama ya teknolojia na kulinda heshima binafsi katika enzi hii ya kidigitali.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button