THRDC yaleta pamoja mashirika ya kiraia, wanasheria

DAR ES SALAAM: MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeandaa mafunzo ya kitaifa ya siku mbili, yakihusisha washiriki 70 kutoka mashirika ya kiraia na mabaraza ya wanasheria kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Mafunzo haya yamefanyika kwa lengo la kuimarisha uwezo wa washiriki katika kushawishi sera, kulinda haki za binadamu, na kupanua wigo wa upatikanaji wa haki kwa kutumia mbinu madhubuti za ushawishi na ushirikiano wa kimkakati.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mratibu wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema mafunzo haya yatasaidia kuongeza uelewa wa washiriki juu ya mbinu bora na za hali ya juu za utetezi wa haki, pamoja na kubaini njia bora za kushirikiana na taasisi za serikali katika kukuza haki na usawa.
Mafunzo hayo pia yamelenga kujenga mitandao imara ya ushawishi wa sera, kushughulikia kesi za kimkakati, kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu masuala ya haki za binadamu na utawala bora. Ushirikiano huu unatajwa kuwa muhimu katika kuhakikisha haki na uwajibikaji vinazingatiwa nchini.
Kwa upande wake, Elimo Massawe, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Dodoma na Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania, ameeleza kuwa mafunzo hayo yatajenga mshikamano na ushirikiano kati ya wadau wa sekta ya sheria na asasi za kiraia.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo utasongesha mbele ajenda ya haki za binadamu na utawala wa sheria kwa mafanikio makubwa.
SOMA ZAIDI: Elimu haki za binadamu kuingizwa kwenye mtaala
Massawe amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja, bega kwa bega, kama mnyororo wa maarifa na uzoefu, huku akihimiza washiriki kujifunza miiko na taratibu za kazi ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mafunzo haya pia yamejumuisha wasilisho muhimu litakaloongozwa na Wakili Kipobota, ambaye atatoa matokeo ya Uchambuzi wa Uhitaji na Pengo la Uwezo kwa mashirika ya kiraia yanayofanya kazi Tanzania Bara na Zanzibar.
Uchambuzi huo unatarajiwa kutoa mwanga juu ya maeneo yanayohitaji kuimarishwa ili mashirika haya yaweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Mafunzo hayo yamewakutanisha wanachama kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Chama cha Wanasheria Zanzibar, Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki, Muungano wa Wanasheria wa Bara la Afrika (PALU), pamoja na ZAFELA. Yamefanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Kuboresha Uwezo wa Ushawishi na Ushirikishwaji.”
Mafunzo haya yanatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika nyanja ya haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Tanzania.