Waomba kesi ya Lissu isiwe ‘live’ wakati wa ushahidi

DAR ES SALAAM; MAWAKILI upande wa Serikali wamewasilisha ombi mahakamani kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu isirushwe live wakati mashahidi wa siri watakapokuwa wanatoa ushahidi wao.
Ombi hilo limewasilishwa leo mahakamani na Wakili Mkuu wa Serikali, Nassor Katuga mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, Franco Kiswaga anayesikiliza shauri hilo.
Akiwasilisha ombi hilo, wakili huyo amedai itakuwa kinyume na amri ya mahakama inayolenga kulinda usalama na utambulisho wa mashahidi hao, kwani watatoa ushahidi kwa siri, hivyo kuwepo matangazo kunaweza kusababisha mashahidi kutambulika kupitia maelezo yao na kuhatarisha ulinzi wao.