Watuhumiwa rushwa kura za maoni CCM matatani

GEITA; TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Geita imethibitisha kupokea na kufanyia kazi viashiria vya rushwa katika mchakato wa kura za maoni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Taarifa ya viashiria vya inatajwa kuripotiwa katika uchaguzi wa kura za maoni Jimbo la Chato Kaskazini na uchaguzi wa wabunge wa viti maalum kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoa wa Geita.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, James Ruge ametoa taarifa hiyo Agosti 14, 2025 mbele ya waandishi wa habari mjini Geita juu ya hatua za ufuatiliaji wa vitendo vya rushwa katika kura za maoni za ubunge na udiwani.
Amesema mnamo Agosti 2, 2025 kuna picha mjongeo ilirushwa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha wajumbe wanawake wakigawana fedha katika Kata ya Nyankumbu Jimbo la Geita Mjini mkoani humo.
Ruge ameeleza tukio hilo linadaiwa kufanyika baada ya kikao cha kuwanadi wagombea ubunge kukamilika na Takukuru ilipata taarifa na kufuatilia kisha kuwatambua, kuwakamata na kuwahoji watuhumiwa.
Ameongeza kuwa mnamo Agosti 4, 2025 ofisi yake ilipata taarifa za chakula na vinywaji kuandaliwa kwa wajumbe wa Jimbo la Chato Kaskazini kata ya Bukome, kijiji cha Buzirayombo katika siku ya upigaji kura.
“Picha mjongeo ya tukio ya tukio hilo ilisambazwa katika mitandao ya kijamii na Takukuru kuinasa, ofisi iliwasaka, kuwakamata kuwashikilia na kuwahoji wahusika,” amesema Ruge.
Ameongeza, kufuatia matukio hayo na mengine yaliyotendeka ofisi ya Takukuru imeanzisha uchunguzi ambapo unakamilishwa kwa kukusanya ushahidi ili kuthibitisha tuhuma za rushwa dhidi ya watuhumiwa.
Ruge amesema mpaka sasa watuhumiwa wote walioonekana kwenye picha mjongeo zilizosambaa wameachiwa huru kwa dhamana kupisha hatua zaidi za uchunguzi na baadaye hatua za kisheria.
Awali akizungumza na waandishi wa habari juu ya tuhuma za rushwa Chato Kasikazini, Katibu wa CCM wilayani Chato, Charles Mazuri alikanusha kupokea taarifa ya vitendo vya rushwa katika kura za maoni.
Amesema maelekezo ya CCM Chato yalitolewa kwenye ofisi zote za kata kuratibu upatikanaji wa huduma rafiki ikiwemo chakula na usafiri kwa wajumbe kutokana na jiografia ya vituo vingi vya kupigia kura.