Wakuu SADC waipongeza Tanzania, Rais Samia

WAKUU wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuimarisha amani na ulinzi katika eneo hilo.

Walitoa pongezi hizo baada ya kupokea taarifa ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Rais Samia kwenye mkutano wa 45 wa kawaida wa wakuu hao Antananarivo, Madagascar juzi.

Katika mkutano huo, wakuu hao walimchagua Rais wa Jamhuri ya Malawi, Dk Lazarus Chakwera awe mwenyekiti wa asasi hiyo na atakapomaliza muda wake atafuatiwa na Mfalme Mswati III wa Eswatini.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alimwakilisha Rais Samia katika mkutano huo.

Katika tamko la pamoja, wakuu hao wa nchi za SADC wameipongeza Tanzania kwa kuandaa kwa mafanikio mkutano wa Afrika kuhusu nishati Januari mwaka huu, Dar es Salaam.

Wameielekeza sekretarieti ya jumuiya hiyo ishirikiane na Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na washirika wengine kusaidia nchi wanachama wa SADC zitekeleze mikakati yake kuhusu nishati hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Mkutano huo ulitoa mwito kwa nchi wanachama zihamasishe ushiriki wa wanawake kwenye michakato ya kisiasa ya utoaji uamuzi, ziimarishe mifumo ya ukusanyaji data na ukusanyaji wa taarifa za mara kwa mara kuhusu unyanyasaji kijinsia.

Wakuu hao walihimiza kuharakishwa uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo SADC kikiwa ni chombo kinachojitegemea cha kuwezesha ustahimilivu wa kiuchumi kwenye eneo hilo.

Pia, mfuko utawezesha maendeleo endelevu na kuhamasisha uwekezaji wa muda mrefu katika programu za SADC.

Mkutano huo ulipitisha na kusaini makubaliano ya kurekebisha Itifaki ya SADC kuhusu fedha na uwekezaji hasa katika vipengele vinavyohusu udhibiti wa utakatishaji wa fedha.

Wakuu hao walihimiza umuhimu wa kilimo ili kuhakikisha kunakuwepo usalama wa chakula. Walitoa mwito kwa nchi wanachama zizingatie mikakati inayoimarisha tija katika kilimo na uwezo wa kukabili mabadiliko ya tabianchi, umwagiliaji na uchumi wa buluu.

Mkutano huo ulimteua Elias Magosi aendelee kuwa Katibu Mtendaji wa SADC kwa kipindi cha pili na cha
mwisho cha miaka minne.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button