SHIMIWI; Miaka 39 ya kutimua vumbi

MASHINDANO ya 39 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) mwaka huu inafanyika kuanzia Septemba Mosi hadi 16 jijini Mwanza.

Mashindano hayo hufanyika kila mwaka katika mkoa uliochaguliwa na mwaka huu Mwanza ndio mkoa uliochaguliwa na kabla ya mashindano hayo, vikao vya maandalizi vimeshaanza ili kuhakikisha yanafanyika kwa mafanikio makubwa.

Ni mashindano yanayoshirikisha wafanyakazi wengi wa wizara na idara mbalimbali na kushirikisha michezo ya mpira wa miguu, netiboli, kuvuta kamba, mbio za baiskeli, drafti na riadha.

Tayari kamati ya kitaifa ya Shimiwi ilikuwa jijini Mwanza, ambako iliendesha mafunzo mbalimbali kwa wasimamizi wa michezo hiyo, ikiwemo kuandaa viwanja vitakavyotumika kuchezea michezo hiyo ambavyo ni CCM Kirumba, Nyamagana, Magereza, shule za Sekondari Nsumba na Nyegezi.

Kwa kawaida, timu inayoshika nafasi ya kwanza hadi ya tatu hupata kikombe lakini katika mchezo wa riadha wenyewe mshindi wa kwanza hadi wa tatu anapewa medali kama ilivyo ada katika mchezo huo.

Kabla ya mashindano hayo ya Shimiwi kufanyika hutanguliwa na bonanza la uzinduzi wa michezo hiyo, ambalo lilifanyika Agosti 2, 2025 kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, ambalo limesaidia kuhamasisha taasisi  kuanza kujiandaa kabla ya kufanyika kwa mashindano hayo muhimu.

Mgeni rasmi wa bonanza hilo alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka, aliyewakilishwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Ikulu, Mululi Majula Mahendeka aliyeagiza uongozi wa Shimiwi kuhakikisha inawasilisha orodha ya wizara, taasisi na ofisi za wakuu wa mikoa ambao hawatashiriki kwenye michezo ya 39 ili zichukuliwe hatua stahiki.

Baadhi ya matokeo ya michezo ya bonanza ni mabingwa watetezi wa mchezo wa kuvuta kamba kwa wanaume, timu ya Ofisi ya Rais Ikulu waliwavuta Hazina kwa mivuto 2-0 huku kwa upande wa wanawake Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) waliwavuta Hazina kwa 2-0 wakati Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Ardhi walitoshana nguvu kwa mvuto 1-1.

Katika mchezo wa netiboli, timu ya Takukuru walilazimishwa sare na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa magoli 25-25 huku Wizara ya Ujenzi waliwachapa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mabao 34-2.

Katika mchezo wa mpira wa miguu, mabingwa watetezi timu ya Utumishi waliwafunga RAS Manyara A kwa magoli 2-0 huku Ikulu wakiwaliza Wizara ya Ujenzi kwa magoli 3-1. Wizara ya Uchukuzi waliichapa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa magoli 2-0 nayo Wizara ya Maji walitoka suluhu na Takukuru huku RAS Manyara B walitoshana nguvu na Takukuru B kwa kutoka suluhu.

Mashindano hayo ni muhimu sana kwani yamewawezesha wafanyakazi kufanya mazoezi na kuimarisha utendaji wao makazini na kupunguza magonjwa yasiyoambukiza ambayo huigharimu serikali fedha nyingi.

Viongozi wa Shimiwi wamewataka waajiri kuwapa wafanyakazi wao muda wa kufanya mazoezi ili waweze kushiriki vizuri kwa timu zao kutoa upinzani.

Shimiwi imeundwa kwa sheria chini ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na kupata uhalali wa kuandaa na kujihusisha na michezo tofauti. Michezo hiyo imekuwa inahusisha  wanamichezo watumishi kutoka wizara, idara, taasisi zinazojitegemea, wakala wa serikali na ofisi za wakuu wa mikoa, likiwa na malengo mbalimbali.

Baadhi ya malengo hayo ni kuwaleta pamoja watumishi hao ili kujenga umoja na mshikamano miongoni mwao, kujenga ukakamavu kwa kuwa na afya bora, kubadilishana ujuzi na kuwafanya wafanye kazi kwa bidii.

Viongozi wa Shimiwi waliopo madarakani hivi sasa ni Daniel Mwalusamba (Mwenyekiti), Michael Masubo (Makamu Mwenyekiti), Alex Temba (Katibu Mkuu), Mariam Kiyange (Katibu Msaidizi), Rose Makange (Mweka Hazina), huku wajumbe ni William Moye, Apollo Kayungi, Tumsifu Mwasamale na Mashaka Mwamage na wajumbe wa kamati ya wanawake ni Itika Mwankenja na Bahati Mollel.

Uongozi huo uliingia madarakani mwaka 2021 kwa uchaguzi mkuu uliofanyika mkoani Morogoro kwa kusimamiwa na kamati ya uchaguzi iliyoteuliwa na BMT, utamaliza kipindi chake cha uongozi mwakani wakati utakapofanyika uchaguzi wa Shimiwi.

Pamoja na michezo hiyo kusimama kwa takribani miaka mitano na kurejeshwa rasmi mwaka 2021 na Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa inasaidia kuimarisha afya za wafanyakazi, kuwaunganisha na kuongeza ari ya utendaji kazi.

Rais Samia akizungumzia michezo ya Shimiwi hivi karibuni aliitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuendeleza michezo na kuhakikisha wizara zote zinashiriki. “Lakini katika mashindano yale wizara na kampuni nyingi huwa hazishiriki, hivyo nakutaka sasa kuhakikisha wizara na mashirika yanashiriki mashindano yale,” alisema.

Rais Samia akitoa maelekezo kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Palamagamba Kabudi, Ikulu, Dar es Salaam hivi karibuni. Vifaa vya Michezo Hivi karibuni Shimiwi ilipata udhamini wa vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh milioni 5.5 kwa ajili ya mashindano hayo yatakayofanyika Mwanza kutoka kwa Kampuni ya Smart Sport chini ya mkurugenzi wake, George Wakuganda.

Katibu Mkuu wa Shimiwi, Temba amesema vifaa hivyo ni jezi, mipira na vikombe kwa ajili ya washindi wa timu za netiboli.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button