Mdau atumia mil 270/- kuboresha miundombinu Muleba

KAGERA: Mdau wa maendeleo wilayani Muleba mkoani Kagera, Ijuka omuka ametekeleza kampeni ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, kwa kurabati miundombinu ya shule kwa kutoa madawati vifaa vya michezo na kujenga visima viwili vya maji kwa wananchi wa vijiji vya Nyarutenge Bilabo na Biija Nyakatanga kwa thamani ya Sh milioni 270.

Miezi kadhaa iliyopita, Fatma Mwassa aliwaalika maelfu ya wakazi wa Kagera akiwataka kukumbuka nyumbani na kufanya shughuli za maendeleo kila mmoja sehemu anayotoka ili kuurudisha Mkoa wa Kagera katika hadhi inayostahili.

Wananchi wa Wilaya ya Muleba wameshuhudia jitihada za makusudi za mzaliwa wa wilaya hiyo, Mosses Kiduduye ambaye ametekeleza kampeini hiyo kwa vitendo kwa kukarabati shule tano kongwe za msingi na kuweka miundombinu katika shule hizo pamoja na kutoa vifaa vya michezo, kukarabati ofisi za walivu na ujenzi wa vyoo ili kuendeleza ushindani wa kielimu katika Wilaya ya Muleba.

Akikabidhi kwa Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dk Abel Nyamahanga Kiduduye alisema kuwa alivutiwa na kampeini ya Mkuu wa Mkoa na katika taswira aliangalia ni kwa jinsi gani anaweza kudunduliza pesa yake na kufanya jambo la kukumbukwa katika jamii yake.

“Mama yangu ni mwalimu nilianza kutembelea shule niliyosomea niliona uchakavu wa miundombinu niliweka malengo na kubaini shule tano kongwe Muleba ,lakini kuna vijiji viwili toka tuzaliwe kuna shida ya maji nako nilisema nitaunga serikali mkono, najisikia faraja kuona nimefanya ushawishi na kukusanya milioni 270 na kuyatekeleza haya yote kama sehemu ya jamii na kuacha alama na kicheko kwa jamii yangu,”alisema Kiduduye.

Amesema serikali imefanya mambo mengi lakini sasa ni wakati wa jamii kufanya mambo mazuri ya kukumbukwa  na zaidi kushirikiana na serikali kuigusa jamii moja kwa moja katika mahitaji yao ambapo alidai kuwa atakuwa mstari wa mbele kushawishi wadau na vijana ili kurudi Nyumbani na kuweka alama zao

Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dk Abel Nyamahanga amefurahishwa na mdau huyo ambapo amekiri kupokea miundombinu iliyoboreshwa katika shule tano za Wilaya ya Muleba ,madawati na vifaa vya michezo pamoja na kupokea miundo mbinu ya maji kwenye visima viwili ambavyo vitahudumia wananchi wengi katika Wilaya ya Muleba.

“Vitabu vitakatifu vinasema mkono unaotoa ndio unaobarikiwa tunawatu wengi sana waliofanikiwa , tuwahimize warudi nyumbani ,warejeshe furaha katika jamii zao zilizowalea ofisi Iko wazi, ni vyema tuendeleze mshikamano na tufanye kitu kwa jamii,pia kwa wilaya yetu nafasi za kuwekeza zipo hivyo wadau wote mje ili Muleba na Mkoa wa Kagera kwa ujumula vingae,”alisema Nyamahanga.

Ofisa Elimu wa Shule za Msingi Wilaya ya Muleba, Angasirini Kwekwa amezitaja shule zilizokarabatiwa  na mdau huyu na kurudi kuwa za kisasa kuwa ni tukutuku shule ya msingi, Kaigara Shule ya Msingi ,Rubungo Shule ya Msingi ,Buyango Shule ya Msingi na Muleba Shule ya Msingi ambapo miundombinu ya shule na ofisi zimekarabatiwa kisasa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button