Mgombea wa Chaumma aja na kipaumbele cha ajira Mafinga Mji

Mgombea ubunge wa Jimbo la Mafinga Mji kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Ngwada Mubarak Twaha, amezindua rasmi ajenda yake ya mapinduzi ya kiuchumi kwa wakazi wa jimbo hilo, akisisitiza kuwa kipaumbele chake cha kwanza, cha pili na cha tatu ni ajira.

Akizungumza baada ya kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jimbo la Mafinga kuwania ubunge, Twaha alisema ameamua kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho ili kupambana na tatizo kubwa la ukosefu wa ajira, hususan kwa vijana wenye shahada za vyuo vikuu ambao wamebaki kukosa mwelekeo licha ya elimu yao.

“Nitahakikisha vijana wenye digrii wasio na ajira wanapata ajira za makusudi na za kudumu. Tunakwenda kuanzisha mfumo wa ajira unaotokana na miradi ya wananchi wenyewe na miradi hiyo itakuwa chanzo cha kodi na maendeleo kwa kila kata,” alisema Twaha.

Twaha alifafanua kuwa mpango wake unahusisha kuanzisha miradi mikubwa ya kiuchumi katika kata zote tisa za Mafinga Mji, ikiwa ni pamoja na kampuni za ujenzi, kampuni za ulinzi, viwanda vya mbao, shule binafsi za walimu, na studio za wasanii.

Mingine ni kuimarisha michezo kwa kuanzishwa kwa timu za mpira wa miguu kila kata, zitakazounda timu ya jimbo itakayojulikana kama Mafinga Mji Shooting, ikishiriki ligi kubwa na hatimaye kupata uwanja wa kisasa utakaovutia mechi za Simba na Yanga.

Mengine ni pamoja na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo – Kupitia wataalamu wa sabuni, mafuta na batiki, wananchi wataanzisha viwanda vyao vidogo kila kata, na Saccos za kata itatumika kuwapatia wananchi mikopo yenye riba nafuu na pembejeo za kilimo.

Twaha alisisitiza kuwa miradi hiyo itaibua walipa kodi wapya na wa kudumu, jambo litakaloongeza mapato ya jimbo na mkoa kwa ujumla.

“Tutawamuru viongozi wa Halmashauri, Wilaya na Mkoa kuhakikisha kazi zote ndani ya kata zinafanywe na kampuni za kata husika, ili pesa ibaki ndani ya jamii,” alisema.

Kwa msisitizo, Twaha aliahidi kusimamia usajili wa kampuni zote kwa mikono yake na kuhakikisha wananchi wanapata faida ya moja kwa moja kutoka kwenye mapato hayo.

“CHAUMMA inakuja kwa nguvu ya ukombozi. Mafinga Mji lazima iwe mfano wa mji unaojiajiri, unaolisha wananchi wake na unaojenga kwa nguvu zake. Huu ndiyo wakati wa mabadiliko ya kweli,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button