Ndoinyo apitishwa, mwingine akiuka kanuni

ARUSHA: MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Ngorongoro kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Arusha, Yannick Ndoinyo amepita bila kupingwa katika kinyang’anyiro cha kuwania kiti hicho baada ya mpinzani wake wa Chama Cha Umma (CHAUMMA) kukiuka kanuni kwa kuchelewa kurudisha fomu ya kuwania ubunge katika jimbo hilo.
Akizungumza kwa njia ya simu, Msimamizi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) katika Jimbo la Ngorongoro, Laban Mchome amesema mgombea wa CHAUMMA Zakhalia Bayo alishindwa kuirejesha fomu yake ndani ya muda uliopangwa na tume hiyo.
Mchome amesema kutokana na hali hiyo INEC imemtangaza mgombea wa CCM kuwa mgombea pekee katika jimbo hilo kwa kuwa mpinzania wake amekiuka masharti ya muda.
‘’Kila mgombe ubunge wakati wa uchukuaji fomu ya ubunge walipewa taratibu zote na nini wanapaswa kufanya ikiwa ni pamoja na kuzingatia muda uliopangwa na INEC wakati wa urudishaji fomu,‘amesema Mchome.
Akizungumzia udiwani katika jimbo hilo,Mchome amesema kuwa wagombea udiwani katika kata 26 kati ya 28 wagombea wa CCM wamepita bila ya kupingwa baada ya kukosa wapinzani.
Mchome alisema kata mbili za Sale na Oldonyosambu wagombea wa CCM walioteuliwa wamepata wapinzani wa Chama Cha Act-Wazalendo katika kata zote.
Act –Wazalendo imemweka,Kabaney Kasey-Mojah kuwania udiwani katika kata ya Oldonyosambu na Kata ya Sale Chama Hicho kimemteua Mussa Radi kuwania udiwani.
Katika Jimbo la Karatu Mgombea ubunge wa Jimbo hilo,Daniel Awack amepata wapinzania watatu wa vyama vya CCK,CHAUMMA,SAU huku mgombea wa TLP alishindwa kuiresha fomu ya kuwania nafasi hiyo na haakukuwa na sababu zozote za kushindwa kuzirejesha.


