Tanzania kuwa kitovu uchumi wa kijani, nishati safi inawezekana

HIVI karibuni, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde wakati akiweka jiwe la msingi la kiwanda cha kusafi sha na kusindika madini ya nikeli na shaba kinachojengwa na Kampuni ya Zhongzhou Mining, eneo la Zamahero wilayani Bahi mkoani Dodoma, alisema Tanzania itakuwa kinara wa mapinduzi ya uchumi wa kijani.

Alisema katika kipindi kifupi kijacho Tanzania inatarajiwa kuwa kitovu cha uchumi huo wa kijani hususani katika utengenezaji wa magari ya umeme, betri za magari, nishati safi na vifaa vya kielektroniki.

Mavunde alisema hatua hiyo itawezekana kutokana na mkakati wa nchi wa kuhakikisha rasilimali madini zinaongezewa thamani ndani ya nchi na kufaidisha Watanzania kupata ajira, kuchangia kodi na mapato ya serikali.

SOMA: Serikali kushirikiana na wadau agenda nishati safi

Hatuna wasiwasi kuwa hili litawezekana kutokana pia na mikakati iliyopo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ambayo pamoja na mambo mengine inazingatia ukuaji wa uchumi na pato la mtu mmojammoja.

Aidha, hatua ya ujenzi wa kiwanda cha Kampuni ya Zhongzhou Mining ni uthibitisho kuwa dhamira ya kuongeza thamani madini nchini iliyobainishwa wazi katika Dira ya 2050 itaipeleka Tanzania kwenye mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa kuteka soko la dunia la bidhaa na teknolojia.

Tanzania ya uchumi wa kijani itaiwezesha nchi kutengeneza magari na vyombo vya kielektroniki nchini na kuongeza thamani madini.

Kama tunakumbuka, katika hotuba na maagizo yake Rais Samia, mara zote akizungumzia sekta ya madini maelekezo yake ni kutaka madini yanayochimbwa hapa nchini yaongezewe thamani ndani ya nchi na kuuza bidhaa ya mwisho badala ya madini ghafi.

Katika kuelekea Tanzania ya uchumi wa kijani, nguvu ya pamoja itahitajika kuchochea zaidi uwekezaji wa viwanda ili miradi mingi zaidi kama huu wa kusindika madini ya nikeli na shaba wa Dola za Marekani milioni 15 utekelezwe nchini.

Kama alivyoeleza Mavunde, mradi huu utakapokamilika utazalisha takribani tani 200,000 za nikeli na shaba kwa mwaka, kuajiri zaidi ya Watanzania 200 hadi 230 na kuchangia kodi na mapato mengine ya serikali.

Hivyo dhamira ya kuifanya nchi kuwa ya uchumi wa kijani, inawezekana.

Tunaamini kupitia Sera ya Madini ya Mwaka 2009 inayoelekeza kuyaongezea thamani madini ndani ya nchi, sheria za madini na miongozo mbalimbali, watendaji katika sekta hii watashiriki kikamilifu ili kufikia malengo haya ya Tanzania ya uchumi wa kijani.

Takwimu zinaonesha hivi sasa Tanzania kuna viwanda vinane vya kusafisha madini ya dhahabu lakini viwanda vya kuongezea thamani madini ya metali vipo tisa huku Dodoma ikiwa navyo vitano.

Hatua hii inatia moyo, lakini kutokana na maendeleo ya teknolojia na ukuaji wa kasi wa uchumi wa Tanzania, nguvu shirikishi italifikisha taifa hili katika mapinduzi makubwa ya uchumi katika muda mfupi ujao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button