Mgombea CHAUMMA Mafinga Mjini awekewa pingamizi

IRINGA: Mgombea ubunge wa Jimbo la Mafinga Mjini kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Ngwada Mubarak Twaha, amewekewa pingamizi la kugombea nafasi hiyo na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dickson Lutevele.

Pingamizi hilo limewasilishwa kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Mafinga Mjini, Doroth Kobelo, likieleza sababu kadhaa zinazodaiwa kumfanya Twaha asistahili kuendelea na mchakato wa kuwania ubunge.

Kwa mujibu wa pingamizi hilo, Twaha anatuhumiwa kuwa si mkazi wa Mafinga Mjini jambo linalomuondolea uhalali wa kugombea nafasi hiyo.

Aidha mgombea huyo anadaiwa kushindwa kukusanya idadi sahihi ya wadhamini kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi kwani orodha yake inaonesha wapo baadhi yao waliofariki na wengine kutoka majimbo mengine ya uchaguzi.

Aidha Lutevele katika maelezo ya nyongeza ameutilia shaka mwenendo wa kisiasa wa mgombea huyo akisema hauna mshikamano.

Lutevele amedai kuwa kila kipindi cha uchaguzi, Twaha amekuwa akibadili vyama vya siasa: mwaka 2010 akigombea kupitia CHAUSTA, mwaka 2015 NCCR-Mageuzi, mwaka 2020 kupitia ACT-Wazalendo, na sasa akitaka kugombea kupitia CHAUMMA.
Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi, Msimamizi wa Uchaguzi amemtaka Twaha ajibu pingamizi hilo ndani ya saa 24 tangu alipokabidhiwa barua husika.

Akijibu kuhusu tuhuma hizo Ngwada amesema sababu zilizotolewa dhidi yake ni za uongo na uzushi na atazijibu zote kwa msimamizi wa uchaguzi kama anavyotakiwa kwa mujibu wa taratibu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button