TCRA yatoa mwongozo SMS za Uchaguzi Mkuu

DAR-ES-SALAAM : MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa mwongozo kuhusu usambazaji wa maudhui na arafa (ujumbe mfupi kwa simu za mkononi) za mkupuo kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari ameagiza wadau wote wahakikishe maudhui wanayopelekwa kwa wananchi yanadumisha umoja, amani na mshikamano wa kitaifa.

Katika taarifa aliyoitoa Dar es Salaam, Dk Bakari amewakumbusha watoa huduma za mawasiliano ya simu na wanaoandaa arafa wahakikishe maudhui mkupuo kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 na baada, yanazingatia sheria na kanuni zote za mawasiliano ya kielektroniki na posta. Dk Bakari ameagiza maudhui yote yanayohusiana na shughuli za Uchaguzi Mkuu yapate idhini kutoka kwa taasisi au uongozi wa chama cha siasa husika.

“Watoa huduma wanapaswa kuhifadhi kumbukumbu za arafa zote zinazotumwa kwa wingi kwa kipindi kinachotakiwa kisheria kwa ajili ya uthibitisho endapo utahitajika,” alisema. SOMA : Vipaumbele 10 vya CHAUMMA kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025

Dk Bakari alisema watoa huduma hao wanatakiwa kuhakiki maudhui kabla ya kusambaza arafa za mkupuo ili kuhakikisha hakuna ujumbe wenye kuchochea vurugu, uvunjifu wa amani au kueneza taarifa za uongo. Ameonya watoa huduma za maudhui mtandaoni wanaosambaza habari na matukio bila kuwa na leseni ya TCRA. Alisema wanaofanya hivyo wanakiuka Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010 na kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020 na marekebisho yake ya mwaka 2022.

Dk Bakari alisema wanaojihusisha na kutoa huduma hizo bila leseni watachukuliwa hatua kali, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya sheria. TCRA ina wajibu wa kusimamia huduma za mawasiliano ya simu na intaneti, posta na utangazaji wa redio, televisheni na maudhui ya mitandaoni.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button