CCK kuunda serikali ya umoja wa kitaifa

DAR-ES-SALAAM : MGOMBEA Urais kupitia Chama cha Kijamii (CCK), David Mwaijojele amesema chama chake kitaunda serikali ya umoja wa kitaifa kama kitapata ridhaa ya kuongoza nchi. CCK imezindua kampeni zake jana mkoani Dar es Salaam katika eneo la Kijichi na kumtambulisha, Masoud Ally Abbdallah kuwa mgombea mwenza wa nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akizungumza wakati wa kuzindua kampeni hizo, Mwaijojele alisema chama chake kina malengo ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa itakayolinda masilahi ya wananchi bila kujali chama. “CCK inakusaidia kuunda serikali na jamii katika taifa lenye misingi ya kidemokrasia, umoja, upendo, haki na matumaini ya maisha bora kwa Watanzania wote,” alisema.

Aliongeza: “Kwa hiyo CCK itakuwa tayari kwa serikali ya umoja wa kitaifa kwa ushirikiano wa vyama vyote bungeni”. Alisema chama hicho kimejipanga na kina sera na ilani bora zaidi ya uchaguzi, akivitaja vipaumbele vyake kuwa ni kutengeneza ajira kwa vijana na wanawake.

Mwaijojele alisema pia chama hicho kimeweka mipango ya kurasimisha upatikanaji wa mikopo kwa wanawake ili kuwaepusha na mikopo umiza. Pia, serikali ya CCK inatarajia kuanzisha mpango wa kujenga nyumba za makazi na kuzipangisha kwa wananchi ili walipe kidogokidogo kwa malengo ya kuwawezesha kumudu gharama za maisha na waishi maisha bora na ya uhakika.

Katika eneo la afya, serikali ya chama hicho italipa gharama zote za matibabu kwa mgonjwa aliyefariki dunia ili kuzuia maiti isizuiliwe hospitalini.  “CCK tutahakikisha sekta ya afya inakuwa vizuri katika maeneo yote kuanzia hospitali za kata mpaka rufaa,” alisema. Katika eneo la madini, Mwaijojele alisema CCK watafanya uwekezaji kwenye vifaa vya uchimbaji wa madini ili wananchi wanufaike na rasilimali zilizopo nchini.

“Tutaboresha miundombinu na vifaa kwenye uchimbaji wa madini, hatuwezi kukubali Tanzania kuitwa masikini wakati nchi ina rasilimali nyingi,” alisema. Kipaumbele kingine ni kwa wafugaji na wavuvi akiahidi serikali yake kuweka mazingira wezeshi kwa wafugaji kufuga kisasa na wavuvi kutumia meli zenye viwango.

Katika hatua nyingine, Mwaijojele aliwanadi wagombea wa udiwani na ubunge wa majimbo ya Mkoa wa Dar es Salaam na leo wanatarajia kufanya kampeni zao Zanzibar. SOMA: Kumekucha kampeni za Uchaguzi Mkuu

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button