Daraja la Tanganyeti likamilike Desemba – Makalla

ARUSHA: Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla leo Septemba 05,2025, ameagiza kukamilka kwa mradi wa Daraja la Tanganyeti lenye urefu wa mita 40 kwenye barabara ya Arusha – Longido – Namanga kuelekea nchi jirani ya Kenya.
Mradi huo unatekelezwa na serikali kwa gharama ya Sh bilioni 4.6 kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD) na Mkandarasi wa Kampuni ya Jiangx Geo Engineering.
CPA Makalla ametoa agizo hilo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua shughuli za utekelezaji wa miradi ya maendeleo Wilaya ya Longido na kumuhimiza mkandarasi wa mradi huo kuongeza kasi na kuhakikisha ujenzi huo muhimu kwa wananchi, unakamilika mwezi Desemba,2025 ili uanze kutoa huduma kwa wananchi.
“Barabara hii ni muhimu kwa uchumi wa nchi hizi mbili za Tanzani na Kenya, hivyo kwa kuzingatia umuhimu wake, ujenzi uendane na kasi ya uhitaji wa huduma kwa wananchi pamoja na wageni wanaotumia barabara hii,”amesema.
Hata hivyo wazee wa Wilaya ya Longido wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa fedha za kujenga daraja hilo kwenye eneo ambalo msimu wa mvua hujaa maji na kusababisha kero kubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mkoa wa Arusha Mzee Michael Lekule Laizer, amebainisha, licha ya Rais kutoa Sh Bilioni 4.6 za kujenga daraja hilo, lakini ametoa fedha nyingi zilizotekelza miradi mikubwa ya afya, elimu maji na mindombinu ya barabara.
Awali aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Longido, ambaye ni Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa amemshukuru Rais Dk. Samia kwa miradi mingi ya maendeleo iliyotekelezwa wilayani humo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake na kumuhakikishia kuwa wananchi wa Longido wanaimani kubwa naye.



