Yupo wapi Anjella? hatimaye aibuka!

DAR ES SALAAM: KUMEKUWA na maswali mengi kutoka kwa wadau wa muziki wa Bongo Fleva wakijiuliza yupo wapi msanii Anjella, aliyewahi kusainiwa kwenye Lebo ya Konde Gang.

Wengi wamekuwa wakibashiri kuwa huenda ameacha muziki, huku wengine wakihisi kuwa huenda ameamua kujikita kwenye shughuli tofauti kabisa.

Ikumbukwe kuwa, baada ya kuondoka Konde Gang, Anjella aliwahi kupewa gari na msanii mwenzake Zuchu kama zawadi. Hata hivyo, muda mfupi baadaye, taarifa zilienea kuwa alikuwa akiugua na hata kuomba msaada wa matibabu ya mguu wake.

Baada ya ukimya wa muda mrefu uliowaacha mashabiki wake na maswali mengi, hatimaye jana kupitia ukurasa wake wa Instagram, Anjella aliweka ujumbe uliotoa taswira ya mwelekeo mpya katika maisha yake.

Msanii huyo aliandika: “Mpe Yesu moyo wako uone atakavyokutendea mazuri.”Aidha, amekuwa akishirikisha mashabiki nyimbo zenye maudhui ya kiroho ikiwemo wimbo wenye maneno “Mtakatifu ni Bwana” hali inayodaiwa kuashiria kuwa sasa ameamua kumtumikia Mungu na kujikita katika maisha ya kiroho.

Hii imewafanya mashabiki wake wengi kuamini kuwa Anjella ameokoka na sasa anaanza ukurasa mpya wa maisha mbali na muziki wa kidunia.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button