AAFP yapongeza vyombo vya habari kwa usawa kampeni uchaguzi mkuu

MGOMBEA urais wa Chama cha Wakulima (AAFP), Kunje Ngombale Mwiru ameisifu hatua kubwa iliyofikiwa na tasnia ya habari kutokana na kuvipa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu usawa na haki kwenye kuhabarisha wananchi.

Kunje ametoa pongezi hizo wakati wa kuhitimisha mwendelezo wa mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Soko la Mawenzi, Manispaa ya Morogoro.

“Waandishi wa habari ni kioo kikubwa cha taifa letu na si kwa taifa letu pekee bali ni pamoja na dunia nzima,”
amesema.

Kunje amesema waandishi wa habari wanaweza kulichonganisha taifa kwa kile wanachoandika kwa vile wananchi wanawaamini kwa yale wanayoandika.

SOMA: Kumekucha kampeni za Uchaguzi Mkuu

“Nitumie fursa hii kuwapongeza waandishi wa habari kwa kuandika taarifa sahihi katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu hususani kwa chama chetu, tangu tumeanza kampeni hii Mkoa wa Morogoro,”amesema.

Mbali na kuwapongeza waandishi wa habari, Kunje amevipongeza pia vyombo vya dola hasa Jeshi la Polisi hususani Mkoa wa Morogoro kwa kufanya kazi zao vizuri.

Kwa upande wa utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi amesema iwapo Watanzania watamchagua katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu kuwa rais, serikali yake itaweka kipaumbele kuboresha sekta ya maji, ikiwamo kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro.

Amesema pia serikali yake itaboresha miundombinu ya barabara kwenye kata zote, upatikanaji wa ajira na itadhibiti mianya inayoingiza wahamiaji haramu hapa nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Vijana wa chama hicho ngazi ya Taifa, Yusuph Rai alisema kuwa katika mwaka ambao chama chake kimepewa nafasi kubwa na vyombo vya habari ni kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025.

“Vyombo vya habari vimeonesha ushirikano tangu tunazindua kampeni Agosti 31, mwaka huu eneo la Kisaki, tumekuwa pamoja eneo la Mngazi, Duthumi, Matombo na hapa Morogoro Mjini,” amesema.

Rai alisema hatua hiyo inawawezesha wananchi kupata habari sahihi za vyama vyote vinavyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na kwamba watakuwa na maamuzi sahihi ya kuchagua chama na mgombea wao katika nafasi ya urais baada ya kuridhishwa na sera zilizonadiwa.

Chama cha AAFP kilizindua kampeni Agosti 31, mwaka huu Kata ya Kisaki, Jimbo la Morogoro Kusini na kuendelea Jimbo la Morogoro Mjini, Kilombero na kitahitimisha katika Jimbo la Kilosa, Septemba 8, 2025.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button