Kiswaga: Dk Samia ameandika historia, Kalenga haitarudi nyuma

Mgombea ubunge wa Jimbo la Kalenga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jackson Kiswaga, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dk Samia Suluhu Hassan imeandika historia ya mageuzi ya maendeleo ambayo wananchi wa Kalenga hawawezi kuyafuta kwa maneno ya siasa za upinzani.

Akizungumza leo mbele ya Rais Samia katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kalenga, Kiswaga alisema wananchi wa jimbo hilo ni mashahidi wa miradi mikubwa iliyotekelezwa ikiwemo barabara, shule, vituo vya afya, pamoja na uwezeshaji wa wakulima kupitia ruzuku za mbolea na miradi ya umwagiliaji.

“Maendeleo haya siyo hadithi, ni mambo yanayoonekana kwa macho. CCM imetekeleza kwa vitendo na sio kwa ahadi hewa. Wananchi wa Kalenga hawatadanganywa tena na wanasiasa wa maneno matupu,” alisema Kiswaga huku akishangiliwa na wananchi.

Aidha, alisema Kalenga ni mfano hai wa kazi kubwa inayofanywa na Dk Samia katika taifa lote, na kwamba Jimbo hilo halina sababu ya kugeuka nyuma wakati maendeleo yanaonekana kwa kasi.

Kiswaga pia aliwasilisha ombi la kuharakishwa kwa usambazaji wa umeme katika vitongoji vilivyobaki na uboreshaji wa barabara ya Wasa, akisisitiza kuwa hatua hizo zitaongeza nguvu ya uwekezaji na ajira kwa vijana wa Kalenga.
Kwa msisitizo, aliwaomba wananchi kumpa Dk Samia kura nyingi za heshima na kuhakikisha kuwa wagombea wote wa CCM wanashinda kwa kishindo.

“Wapinzani wanakuja na maneno, lakini sisi CCM tunakuja na kazi zilizothibitishwa. Kalenga haiwezi kurudi nyuma, kazi iendelee!” alisema Kiswaga.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button