Samia atoa ahadi 5 uchumi Igunga
MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ametoa ahadi tano ambazo zitasaidia kuchochea biashara na uchumi wa wananchi Igunga mkoani Tabora.
Samia amesema hayo wakati wa mkutano wa kampeni katika Wilaya ya Igunga.
Amesema wananchi wakimchagua serikali yake itajenga kituo cha mabasi cha kisasa na soko la kisasa ili kuongeza wigo wa biashara na kuvutia uwekezaji.
Samia pia ameahidi kujenga barabara za lami zinazopita maeneo ya uzalishaji wa mpunga, mbaazi, dengu na choroko na madini ili kuongeza kasi ya kukuza uchumi.
SOMA: CCM yafunika Dar, Samia aahidi makubwa siku 100 ofisini
Ameahidi pia kujenga kituo cha kupokea na kupooza umeme kwa kuwa Igunga ina mahitaji makubwa ya nishati ya umeme hasa ikizingatiwa serikali yake itaanzisha kongani ya viwanda kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao.
Samia ameahidi kuja na njia sahihi ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ambao wamekuwa kero kwa wananchi wa vijiji vinavyopakana na hifadhi.
Pia, ameahidi kuendelea kuimarisha huduma za kijamii za afya, maji na elimu hasa kutokana na kuwepo kwa uhitaji wa huduma hizo kwa wananchi pamoja na kuwa kazi kubwa imefanyika.
“Ili tuyafanye haya na mengine ambayo yako kwenye ilani ya uchaguzi kwa Igunga ni lazima ushindi kwa CCM. Sina mashaka na Igunga kuwa tutapata ushindi tunachotaka sio ushindi pekee bali ushindi wa heshima ili kuwazibe midomo wale wengine,” amesema Samia.
Iramba
Awali, katika mkutano wa kampeni wilayani Iramba mkoani Singida ameahidi kutoa kupaumbele kwa wachimbaji wadogo wa madini.
Pia, ameahidi kuendelea na utafiti wa mafuta na gesi katika kitalu cha Eyasi-Wembele mradi ambao utawavutia wawekezaji katika eneo la Iramba, Igunga na Meatu.
Samia amesema serikali iliahidi uanzishwaji soko la madini na lilianzishwa Shelui wilayani Iramba na tayari zaidi ya gramu milioni 1.5 zimeuzwa kwa thamani ya Sh bilioni 192.
“Hii ina maana Shilingi bilioni 192 zimeingia mikononi mwa wachimbaji ndani ya wilaya hii ya Iramba na soko lile linaendelea kutoa huduma,” amesema.
Samia amesema serikali iliahidi kutoa kipaumbele kwa wachimbaji wadogo ambapo tayari maeneo yaliyohodhiwa na waliokuwa hawayatumii leseni zake zimefutwa.
Amesema leseni hizo zilifutwa na wamepewa wachimbaji zikiwemo 32 zilizotolewa kwa vikundi tisa ndani ya Wilaya ya Iramba kwa wachimbaji wadogo wa madini na nane za uchenjuaji madini ya dhahabu zimetolewa katika eneo la Sekenke.
Samia amesema serikali yake imeweka mazingira mazuri kwa wachimbaji wa madini ikiwamo kuwapelekea nishati ya umeme na kuahidi kuendelea kufanya hivyo.
Afya, elimu
“Kwenye afya tumefanya mambo mazuri lakini bado tutaendelea kwa sababu mahitaji bado yapo, tutaendelea na ujenzi wa vituo vya afya, ujenzi wa zahanati lakini kubwa zaidi kusimamia upatikanaji matibabu na dawa kwa wananchi,” alisema.
Samia amesema serikali itaanza majaribio ya bima ya afya kwa wote na bado kuna maradhi ambayo kwa wale wasiokuwa na uwezo serikali itakwenda kugharimia.
“Wale wasiokuwa na uwezo serikali itakwenda kugharamia kwa asilimia 100, kama mkulima wa choroko, mbaazi na dengu, umeuza na fedha ipo, tunakutaka ununue bima yako ya afya, lakini kwa wale ambao hawana uwezo kabisa serikali inakwenda kusimamia wananchi wake,” amesema.
Samia alisema katika elimu serikali imejenga vyuo vya ufundi na itaendelea kujenga shule kadri mahitaji yanavyoongezeka katika sekta ya maji aliahidi kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji nchini ukiwemo mradi wa maji wa miji 28 na uchimbaji wa visima.
Ameahidi pia kutekeleza kwa haraka mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria hadi Dodoma.
“Tukimaliza uchaguzi na mkitupa ridhaa ya kuendesha serikali namkaba Mwigulu (Nchemba) azitafute fedha za kutekelezea mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria hadi Dodoma, mradi ule utakwenda kumaliza shida zote. Sasa fedha tutatoa wapi ni mimi (Samia) na yeye (Mwigulu) tutajua tunazipata wapi,” amesema.
Samia amesema kwa upande wa Iramba Mashariki serikali itakamilisha ujenzi wa mradi mkubwa wa umwagiliaji katika Kijiji cha Ishishi, Kata ya Msingi kwa gharama ya Sh bilioni 34 ili wakulima walime mara mbili kwa mwaka.
Amesema serikali itajenga barabara za Iguguno mpaka Sibiti na barabara ya Kiomboi hadi Mtulia kwa kiwango cha lami.



