SAU: Tutainua wazawa, tutailisha Afrika

CHAMA cha Sauti ya Umma (SAU) kimesema ndani ya miaka mitano, serikali yake itazalisha ajira milioni 10 katika sekta za kilimo, viwanda, teknolojia na vipaji.

Mgombea urais kupitia chama hicho, Majalio Kyara amesema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni za SAU kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu, Ukonga Mombasa mkoani Dar es Salaam.

Kyara amesema serikali yake itafungua uchumi kwa kuruhusu wazawa kuwekeza kwenye miradi yote mikubwa ya maendeleo.

Amesema kama wazawa hawatakuwa na uwezo, kila mwekezaji wa kigeni atalazimika kushirikisha Mtanzania kwa angalau asilimia 30 ya umiliki.

SOMA: Kampeni za uchaguzi ziwe za kistaarabu

Kyara alisema SAU itafungua kongani ya viwanda na itajenga sekta ya viwanda inayostawi, inayoongeza fursa za ajira na kuimarisha uchumi.

“Viwanda vya nguo, usindikaji wa nyanya, bidhaa za ngozi na mazao mengine vitapewa kipaumbele ili kuongeza thamani ya malighafi na kuhakikisha tunalishika soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC),” amesema.

Kyara amesema serikali yake itarejesha heshima ya kilimo kwa kukifanya msingi wa uchumi na chanzo cha kuimarisha afya za wananchi.

“Tumekusudia si tu kulisha Tanzania bali pia Afrika. Tutaleta mabadiliko yanayokwenda na wakati bila kuacha uhalisia, sambamba na kuboresha maisha ya wakulima na kuhakikisha usalama wa chakula kwa taifa. Tunataka kilimo kiwe cha kisasa, endelevu na chenye faida stahiki kwa wakulima,” amesema.

Kyara amesema serikali ya SAU itazingatia kilimo kisichotumia kemikali kwa kurejesha mbegu za asili ili kulinda afya za wananchi na kuimarisha kilimo hai ambacho ni salama kwa mazingira.

Amesema kila kipande cha ardhi nchini lazima kitumike kuzalisha na mashamba makubwa yasiyoendelezwa yatagawiwa kwa wananchi wenyeji wenye nia ya kuyaendeleza.

Kyara amesema serikali ya SAU itajenga mabwawa 70 makubwa yatakayohudumia zaidi ya ekari milioni 1.4 za kilimo cha kisasa na pia yatatumika kwenye uvuvi na kuzalisha tani 28,000 za samaki kwa mwaka.

“Kupitia uwepo wa maji tutawavuta wawekezaji wakubwa wa kilimo duniani kushirikiana na wananchi katika kuzalisha chakula kingi kitakachotosheleza mahitaji ya ndani na kuuza nje ya nchi,” amesema.

Kyara amesema chama chake kitaanzisha mifumo ya mikopo yenye riba nafuu na ya muda mrefu kwa vikundi vya wakulima, hasa vijana, wanawake na walemavu wanaolima zaidi ya ekari 30 ili wanunue zana za kisasa, pembejeo, kujenga maghala na viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, uvuvi na mifugo.

Naye mgombea mwenza wa chama hicho, Satia Bebwa alisema teknolojia itakuwa uti wa mgongo wa maendeleo ya taifa. Hivyo, serikali ya SAU itawekeza kwenye miundombinu ya kidijiti ili kuwawezesha vijana kushindana katika uchumi wa dunia.

“Huu ni wakati wetu kuinuka pamoja kwa nia moja ya kujenga mustakabali ambao kila mmoja anaweza kujivunia. Ungana nami kwa Tanzania ambayo kila mwananchi anaitamani,” amesema Bebwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa SAU, Bertha Mpata alisema chama hicho kina dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo, mshikamano wa kitaifa na kulinda muungano wa nchi na Afrika kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button