Mamlaka Tanzania, Algeria zajadili kuinua sekta ya petroli, gesi asilia

ALGIERS, ALGERIA: Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli nchini (PURA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Petroli Algeria (ARH) zimekutana na kujadiliana uanzishwaji wa mashirikiano yatakayowezesha kubadilishana uzoefu wa udhibiti wa masuala ya kiufundi ya shughuli za mafuta na gesi.

Majadiliano hayo yamefanyika Septemba 09, 2025 katika ofisi za ARH jijini Algiers, Algeria na kuhudhuriwa na viongozi na maafisa waandamizi kutoka taasisi hizo akiwemo mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Shigela Malosha na Kaimu Raisi wa ARH, Samir Houghlaouene.

Kupitia majadiliano ya kikao hicho, miongoni mwa maeneo ambayo PURA na ARH zinalenga kubadilishana uzoefu ni pamoja na ukaguzi wa mitambo na vifaa vinavyotumika katika miradi ya mafuta na gesi; na uandaaji wa kanuni zinazoongoza shughuli za mafuta na gesi.

Akizungumza katika majadiliano hayo, Shigela alieleza kuwa suala la kubadilishana uzoefu baina ya taasisi hizi ni muhimu na zitawezesha PURA na ARH kujifunza namna bora ya kusimamia masuala ya kiundi hatua itakayowezesha kuongezeka kwa ufanisi wa utendaji.

SOMA: Balozi, bosi Sonatrach wateta fursa za uwekezaji sekta ya mafuta, gesi asilia 

“Kwa kuwa PURA na ARH zote zinadhibiti masuala ya kifundi katika miradi ya mafuta na gesi inayotekelezwa na kampuni katika nchini zetu, ni dhahiri kuwa kwa taasisi zetu kubadilishana uzoefu wa namna tunavyotekeleza jukumu hili kutawezesha kuboresha ufanisi na kuongeza tija katika sekta” alieleza Shigela.

Kwa upande wake, Kaimu Raisi wa ARH, Samir alisema kuwa, ubadilishaji wa uzoefu kati ya PURA na ARH ni muhimu kwa ustawi wa sekta ya mafuta na gesi nchini Tanzania na Algeria kwa kuwa usimamizi makini wa shughuli za kiundi ni moja ya jukumu muhimu katika utekelezaji wa miradi ya mafuta na gesi.

“Kama wadhibiti, kubadilishana uzoefu wa usimamizi wa masuala ya kiufundi ni suala la msingi na litasaidia kujifunza na kuweka katika matendo mambo mazuri ambayo mamlaka zetu zinatekeleza katika eneo hili. Kwa kufanya hivyo, miradi ya mafuta na gesi inayotekelezwa itakuwa endelevu” aliongeza Samir.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button