Mkakati wa kitaifa unahitajika kukabili vitendo vya kujiua

TATIZO la watu kujiua limeendelea kuitesa jamii na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imethibitisha hali hiyo wakati wa maadhimisho ya Siku ya kuzuia kujiua duniani baada ya kubainisha kuwa tatizo la kujiua si suala la kiafya pekee bali pia ni changamoto ya kijamii na kiuchumi inayogusa kila sekta ya Taifa.
Kwa mujibu wa Mkurungenzi Mtendaji wa MNH, Dk Delilah Kimambo tatizo hili mara nyingi hufunikwa na ukimya, unyanyapaa na kutoelewa, lakini kumbe nyuma ya kila takwimu kuna hadithi ya kibinadamu huenda ni mama, baba, kaka, dada, mwanafunzi au jirani aliyepoteza matumaini au simulizi za maumivu na upweke.
Hata takwimu za dunia zinathibitisha tatizo kuwa kubwa kwani zinaonesha zaidi ya watu 720,000 hufariki kila mwaka kwa kujiua ikimaanisha maisha ya mtu mmoja hupotea kila baada ya sekunde 40 na asilimia 90 ya vitendo vya kujiua vinatokana na magonjwa ya afya ya akili.
SOMA: Dalili, namna ya kusaidia anayetaka kujiua
Kwa takwimu hizi ni udhihirisho kuwa kuna kazi kubwa inahitajika katika jamii ya kiroho na kimwili ili kukabiliana na changamoto hii inayosababisha watu kukatisha maisha na mara nyingine kwa kukosa tu msaada wa mawazo ya namna ya kukabiliana na yale wanayoyapitia katika maisha.
Tunaamini ili kukabiliana na hali hii ya watu kujiua na wengine wengi kujaribu kujiua, kuna haja ya kuweka mifumo madhubuti ya kitaifa inayojumuisha sera, bajeti ya kutosha na mifumo thabiti ya utekelezaji.
Kuna haja ya sera kwa sababu tunaamini itasaidia kuleta mwongozo rasmi unaoonesha dhamira ya serikali au taasisi katika kushughulikia tatizo hilo.
Iwapo kutakuwa na sera pia itasaidia kujenga uelewa kwa jamii kwa kuanzisha kampeni za kitaifa za kuelimisha umma, kupunguza unyanyapaa dhidi ya watu wenye changamoto ya afya ya akili na kujiua, sambamba na mamlaka husika kuchukua hatua madhubuti.
Tunaamini ikitengwa pia bajeti itawezesha kuwa na fungu maalumu la kugharamia huduma za afya ya akili na kusaidia jamii bila ubaguzi.
Mfano ikiwepo bajeti itakuwa rahisi hata kutekeleza programu za kuzuia kujiua kwa maana ya kuanzaisha vikundi vya ushauri nasaha mashuleni, kutoa msaada kwa mawasiliano ya simu au mitandao ya kijaamii au kuendesha kampeni za uelimishaji.
Vilevile matumaini yetu ikiwepo mifumo mizuri itasaidia kutekeleza sera na kutumia bajeti iliyotengwa kwa ufanisi. Mifumo ikiwepo pia itasaidia kuhakikisha huduma zinapatikana kwa watu wa makundi yote, mijini na vijijini bila kubagua.
Tunaendelea kusisitiza kuwa ili kupunguza na kuzuia vifo vinavyotokana na kujiua ni muhimu kuwa na mkakati wa kitaifa unaojumuisha sera madhubuti, bajeti ya kutosha na mifumo thabiti ya utekelezaji.
Kwa sababu kwa juhudi za mtu mmoja mmoja au taasisi binafsi pekee haziwezi kuleta mabadiliko ya kweli, hivyo tuiombe serikali na jamii kwa ujumla kuwajibika na kuhakikisha suala la afya ya akili linapewa kipaumbele sawa na afya ya mwili na kila mtu anapata msaada wa haraka kabla ya kufikia hatua ya mwisho ya kujiua.